Dar es Salaam. Serikali imesema imebaini uwepo wa ongezeko la watu wenye dalili za homa, kukohoa, mafua, kubanwa kifua na maumivu ya mwili kwa kipindi cha Desemba 2021 hadi Machi 25, 2022.
Ongezeko hilo limekuwa likitokea katika kipindi cha mwishoni na mwanzoni mwa mwaka kwa miaka mitatu mfululizo ambapo imekuwa ikipungua mwaka hadi mwaka.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumatano Machi 30, 2022 na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Aifelo Sichwale imeeleza kuwa Serikali imebaini uwepo wa kirusi cha Infuenza ambapo kati ya sampuli 1,843 zilizopimwa kwa kipindi cha 12 Desemba 2021 hadi 13 Machi 2022 sampuli 53 ambayo ni sawa na asilimia tatu zilionekana kuwa na virusi vya Influenza A vinavyosababisha mafua makali na nimonia.
“Kirusi hiki kimekuwepo hapa nchini kwa muda mrefu na siyo kirusi kipya, kiwango cha maambukizi ya kirusi hiki kinaonesha kupungua ukilinganisha na miaka ya nyuma ambapo kilikuwa cha wastani wa asilimia 5 hadi 6.
“22 hadi 25 Machi 2022 wizara ilituma timu ya wataalam katika mkoa wa Dar es Salaam kupitia katika vituo vya kutolea huduma za afya ili kufuatilia magonjwa haya ya mfumo wa njia ya hewa kwa watoto waliokuwa wamelazwa wenye umri chini ya miaka 12.
Takwimu zilizokusanywa zinaonesha ongezeko la wagonjwa wenye dalili za homa, kukohoa, mafua, kubanwa kifua na maumivu ya mwili tangu Desemba 2021 hadi 25 Machi 2022, ingawa takwimu hizo zilionesha kupungua kulinganisha na kipindi kama hicho mwaka uliopita” imeeleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa katika ufuatiliaji huo sampuli 123 zilichukuliwa kwa watoto wenye dalili hizo ambapo sampuli 16 kati ya 123 ambayo ni sawa na asilimia 13 zilikuwa na virusi vya mafua ya influenza A.
“Sampuli zote hizo hazikuwa na Uviko-19, kiwango hiki cha asilimia 13 ni kikubwa ukilinganisha na kile cha wastani wa asilimia tano hadi sita ambacho kimekuwepo hapa nchini kwa muda mrefu.
“Kiwango hiki inawezekana ndicho kilichopelekea ongezeko la watu hasa watoto wenye dalili tajwa katika vituo vya kutolea huduma za afya hususani katika mkoa wa Dar es Salaam” imeeleza taarifa hiyo.