Dar es Salaam. Shahidi wa tatu katika kesi ya mauaji inayomkabili Miriam Mrita, mke wa marehemu bilionea Erasto Msuya na mfanyabiashara Revocatus Muyella, ameieleza Mahakama alivyoshuhudia damu ikiwa imetapakaa ulipolala mwili wa marehemu Aneth Msuya, huku ukiwa amezibwa kitambaa sehemu za siri.
Mwanaisha Khassan (27), shahidi wa tatu wa Jamhuri katika kesi hiyo, alidai mtoto wa marehemu huyo, Allan Kimario (4) ndiye aliyemchukua na kwenda kumwonyesha mama yake alipolala.
Mrita na Muyella wanashtakiwa kwa kumuua kinyama Aneth Msuya Mei 25, 2016 huko Kibada, Kigamboni, Dar es Salaam.
Shahidi huyo (27) mkazi wa Kibada Kigamboni alieleza hayo jana wakati akitoa ushahidi wake katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, akiongozwa na Wakili wa Serikali Caroline Matemo, mbele ya Jaji Edwin Kakolaki.
Alidai akiwa nyumbani kwake majira ya saa mbili asubuhi alifika mtoto wa marehemu Aneth, Allan na kumweleza kuwa hamwoni mama yake na alipomchukua mtoto huyo kumrudisha nyumbani kwao alikuta geti likiwa wazi.
“Allan alikuwa akiishi na mama yake na msichana wa kazi lakini siku hiyo msichana hakuwepo. Baada ya kufika niliingia ndani na kukuta mlango upo wazi. Niligonga lakini hakuna aliyeitikia.
“Allan alinichukua na kuniingiza chumba ambacho mama yake alikuwa analala. Kabla ya kuingia nilibisha hodi lakini hakuna aliyeitikia. Allan alinivuta na kunionyesha mama yake akiwa amelala chini,” alisema shahidi huyo.
Alidai baada ya kuingia alikuta mwili wa Aneth ukiwa uchi umelala chali na umefungwa kitambaa usoni na kingine kikiwa kimewekwa sehemu za siri, huku eneo alilolala likiwa limeenea damu.
“Nilishtuka nikamchukua mtoto na kuondoka naye, nilitoka nje na kuomba msaada kwa wamama waliokuwa wanapika mama ntilie kwa nje nao walienda kuangalia, baada ya hapo sikujua kilichoendelea.”
Naye shahidi wa nne, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Richard Mwaisemba (48) aliieleza Mahakama namna alivyopata taarifa ya mauaji akiwa Kituo cha Polisi Kigamboni.
(Wakati tukio hilo likitokea alikuwa Mkuu wa Upelelezi (OC-CID) Wilaya ya Kigamboni. Hivi sasa ni Mkuu wa Polisi wilaya ya Mkalama mkoani Singida).
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Genef Tesha, Mwaisemba alidai Mei 26, 2016 saa moja asubuhi akiwa Kituo cha Polisi Wilaya Kigamboni alipigiwa simu na Mkuu wa Kituo cha Polisi Kibada na kumueleza taarifa za mauaji hayo.
“Baada ya kupata taarifa nilikusanya askari na kuelekea Kituo cha Polisi Kibada. Nilipofika nilikuta wakinamama wengi, baadhi waliingia kwenye gari na kwenda nao eneo la tukio,” alidai shahidi huyo.
Alidai kuwa alipofika eneo la tukio yeye na askari wengine wawili na Mwenyekiti wa eneo hilo, waliingia ndani na askari wengine walibaki nje.
“Baada ya kuingia tulikuta mwili wa mwanamke umelala chali damu zikiwa zinatoka, na pembeni kukiwa na nguo ya ndani (chupi) pamoja na kisu.
“Kwa hali ile niliwaambia wenzangu inabidi kuleta wataalamu wa kitengo cha uchunguzi ambacho kipo chini ya RCO wa Temeke,” alisema shahidi huyo.
Alidai mlango wa mbele wa nyumba lilipofanyika tukio ulivunjwa kwa tofali kutokana na vipande vilivyokuwepo chini.
Mashahidi wanne wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi kati ya 45 wanaotarajiwa kuitwa.