Shekhe Ponda Issa Ponda
KATIBU Mkuu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda ametoa wito kwa Watanzania kuacha malumbano yanayomhusu Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Sheikh Ponda ametoa kauli hiyo leo tarehe 5 Machi, 2022 siku moja baada ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu kuachiwa huru jana tarehe 4 Machi.
Mbowe na wenzake walifutiwa mashtaka yote ya ugaidi yaliyokuwa yakiwakabili katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi baada ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali, DPP, kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na shauri hilo.
Aidha, akizungumzia hatua hiyo, kupitia ukurasa wake wa Twitter leo, Sheikh Ponda ameandika;
“Mh. Mbowe amekuwa huru. Kongole waliopaza sauti, kongole DPP na kongole Mbowe kwa ukomavu wa kisiasa. Kwa hapa tulipofika, nashauri malumbano yaliyohusu Mbowe na Zitto yaachwe, hayana faida yoyote. Tuimarishe nguvu ya pamoja kutafuta mustakbali bora wa Taifa.”
Kauli hiyo ya Sheikh Ponda imetokana na kauli ya Zitto aliyoitoa jana kwamba pamoja na kufarijika kuwa Mbowe ameachiwa huru, lakini hatua hiyo ni mafanikio ya Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) ambacho Zitto ni Mwenyekiti wake.
“Mtakumbuka maoni tuliyoyatoa wakati wa mkutano wa Rais Dodoma, niliitwa kuzungumza kwa niaba ya TCD niliomba viongozi wote tuwepo.
“Miezi sita iliyopita wakati tunaanza shughuli ya kuhakikisha TCD inafanya majukumu yake inavyotakiwa, Rais alikuwa hajakutana na vyama, amekutana na vyama… kuna vyama vilileta malalamiko kwenye vikao vya TCD kuhusu viongozi kutokuwa huru, kuwa magereza, wametoka magereza, nini cha zaidi!
Kauli hiyo ya Zitto iliibua mijadala miongoni mwa wanasiasa, hasa ikizingatiwa katika
Mkutano wa Wadau wa Kujadili Hali ya Demokrasia ya Vyama Vingi Nchini uliofanyika tarehe 15 Desemba, 2021 ambao Zitto alishiriki, baadhi ya vyama vya siasa ikiwamo Chadema, vilisusia mkutano huo.
Hata hivyo, mijadala iliibuka zaidi baada ya Zitto kupewa nafasi ya kuzungumza katika mkutano huo na kumuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuwasaidia kumtoa Mbowe ili waungane naye katika kujenga taifa.
Ombi hilo la Zitto kwa Rais Samia wakati huo lilizidi kuibua mabishano kati ya makada wa Chadema na Zitto kwa madai kwamba Kiongozi huyo wa ACT Wazalendo aliwasaliti kwa kushiriki mkutano huo lakini pia akaisemea Chadema kwa kuwaombea msamaha mithili ya Mbowe na wenzake walikuwa na hatia jambo ambalo halikuwa limefikiwa tamati mbele ya Mahakama.