DAKIKA 90, za mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika zimemalizika kwa wenyeji ASEC Mimosas kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 katika Uwanja wa General Mathieu Karekou.
Mabao ya ASEC Mimosas yamefungwa na Aubin Kramo dakika ya 16, Stephane Aziz Ki aliyefunga bao safi kwa shuti kali dakika ya 25 ya kipindi cha kwanza cha mchezo huku Karim Konate akifunga la tatu dakika ya 57.
Licha ya Simba kupoteza mchezo huo ila kipa wake, Aishi Manula aliibuka shujaa baada ya kuokoa penalti mbili za Karim Konate dakika ya 36 na Anicet Alain Oura dakika ya 90 ya mchezo baada ya beki Joash Onyango kufanya madhambi.
Mabadiliko yaliyofanywa kipindi cha pili na kocha Pablo ya kuwaingiza, Bernard Morrison, Peter Banda, Taddeo Lwanga, Chris Mugalu na Pascal Wawa yalionekana kuleta tija zaidi tofauti na ilivyokuwa kipindi cha kwanza.
Katika matokeo mengine ya kundi hili Gendarmerie nationale ya Niger imefungana mabao 2-2 na RS Berkane ya Morocco.
Msimamo wa kundi hili baada ya mechi tano kupigwa, ASEC Mimosas inaongoza kwa pointi tisa, RS Berkane na Simba zinashika nafasi ya pili na tatu kwa pointi saba, huku Gendarmerie nationale ikishika mkia na pointi tano.
Mchezo wa mwisho ambao utaamua hatima ya Simba kutinga hatua ya makundi utapigwa AprilI 3, dhidi ya Gendarmerie Nationale katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.