KIKOSI cha Simba SC ambacho kwa sasa kipo Benin kwa ajili ya kucheza dhidi ya ASEC Mimosas leo
Jumapili, unaambiwa ulinzi waliowekewa ni wa kiwango cha juu.
ASEC kutoka Ivory Coast, ndiyo wenyeji wa mchezo huo wakitumia Uwanja wa l’Amitié uliopo jijini
Cotonou nchini Benin kwa mechi zao za nyumbani baada ya viwanja vya kwao Ivory Coasta kuwa kwenye marekebisho.
Mchezo huo wa Kundi D wa Kombe la Shirikisho Afrika, utachezwa kuanzia saa 1:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
Akizungumza na Spoti Xtra, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema: “Naomba nisema tu kuwa, baada ya kikosi kufika hapa Benin jana (juzi Ijumaa mchana), wachezaji wote walipata muda wa kupumzika kidogo, kisha jioni wakaenda mazoezini kuweka miili sawa.
“Cha kufurahisha zaidi tumepewa ulinzi mkubwa mno, huku tukifikia kwenye hoteli ambayo ipo karibu na Ubalozi wa Tanzania. Hapa hakuna mwamko mkubwa wa soka, yani wenyeji kama vile hawafahamu kitu kuhusu mechi yetu ukizingatia kwamba wote ni wageni, sio ASEC wala sisi.”
Wakati huohuo, mmoja wa watu waliosafiri na kikosi cha Simba, amelitonya Spoti Xtra kwamba: “Tulipofika Benin,
tulipokewa vizuri sana, ulinzi ni wa uhakika.
“Tulisindikizwa na pikipiki mbili za kijeshi, halafu ndani ya gari tukakabidhiwa polisi wanne, wengine wawili
wakiwa ni wa kampuni binafsi.”
Katika mchezo wa kwanza uliopigwa Dimba la Mkapa, Dar, Simba ilivuna ushindi wa mbao 3-1 dhidi ya ASEC.
STORI: MUSA MATEJA, DAR ES SALAAM