SIMBA wamesisitiza kwamba wanajua chakufanya ndani ya siku 10 kuanzia leo kabla ya kucheza mechi muhimu ya kufuzu robofainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya USGN Jijini Dar es Salaam.
Uongozi umesisitiza kwamba ndani ya muda huo watajipanga vizuri ndani na nje ya Uwanja na wameshazungumza kwa kirefu na wachezaji na benchi la ufundi kila mmoja ameahidi kupambana.
Mechi ya awali, Simba na USGN zilitoka sare ya bao 1-1, Simba ikivuna pointi moja ugenini, ambayo mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema kupata pointi ugenini ni faida kwao.
“Nyumbani tutapambana tunapata matokeo mazuri na kufuzu, huo ndio mpango na ndoto ya kila Mwanasimba msimu huu,” alisema Try Again jana na kusisitiza kwamba kuna kiasi cha fedha wamewaahidi wachezaji ambacho ni siri ili kufanikisha ushindi mnono kwenye mechi hiyo muhimu kwa klabu na Taifa.
Nahodha wa Simba, John Bocco amewataka wachezaji wenzake kuyaacha ya Benin na kutazama yajayo ambayo ndio yatatoa taswira ya wao kusonga mbele au kusalia walipo.
“Kufungwa kunaumiza, lakini ndio mpira, hakuna namna tunatakiwa kuangalia yaliyoko mbeleni sasa, nawapongeza wachezaji wenzangu walipambana kupata matokeo lakini ndio mpira bahati haikuwa kwetu,” alisema Bocco ambaye ni staa wa zamani wa Azam na miongoni mwa wachezaji wazoefu wa mechi kubwa nchini Tanzania kuanzia levo ya timu za Taifa mpaka klabu.
MAKOCHA WASHAURI
Baadhi ya makocha nchini wamemshauri kocha Pablo Franco njia za kupita ili kutoboa kwenye mchezo wao wa mwisho wa kuamua hatma ya Kundi D April 3.
Simba iko nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi hilo ikiwa na pointi saba sawa na RSB Berkane, huku ASEC ikiongoza kundi na pointi tisa.
Nafasi ya kufuzu kwenye kundi hilo ipo wazi ikitegemea na matokeo ya mechi za mwisho, ambayo kama Simba itashinda itatinga robo fainali sanjari na mshindi wa mechi kati ya RSB Berkane na ASEC ambayo hata ikipata sare inafuzu.
Ugumu wa kundi hilo umewaibua baadhi ya makocha ambao wamemshauri kocha Pablo kuwa makini zaidi katika maeneo matatu kwenye mchezo wa mwisho Simba ikicheza nyumbani.
“Kocha anapaswa kuwa mnyumbufu katika kubadili mchezo, hicho ndicho kikubwa,” alisema kocha Francis Baraza wa Kagera Sugar na kuongeza:
“Abadili mfumo wake uwanjani kulingana na wapinzani wao watakavyokuwa,hiyo ni mechi ya kufa na kupona kwa Simba, japo naamini kwa aina ya wachezaji alionao na mkakati wa klabu yao kuwa kwa Mkapa hatoki mtu, Simba itapata matokeo mazuri na kufuzu kucheza robo fainali.”
Alisema kingine ni Simba kutocheza mchezo wa wazi, jambo ambalo anasema lilichangia kuigharimu timu hiyo kwenye mechi iliyopita na ASEC wakapoteza kwa mabao 3-0 ugenini.
“Mechi iliyopita Simba ilicheza wazi sana , hicho ndicho kilichangia wakaadhibiwa, lakini kwa ubora, rekodi na uwezo wa Simba, bado nafasi ya kufuzu kwao ni kubwa zaidi,” alisema
“Simba inawachezaji wengi wa kubadili matokeo, Bernard Morrison ni miongoni mwao, kocha anafahamu nini anakwenda kufanya, ila akiweza awe na mifumo hata mitatu kwenye mechi hiyo na abadilike kutokana na namna wapinzani wao watakavyokuja.”
Kocha Fred Felix Minziro alisema bado nafasi ya Simba kufuzu ni kubwa kama wataitumia mechi yao ya nyumbani vema akisisitiza kwamba uzoefu wa timu hiyo kwenye mashindano hayo kunaipa nafasi ya kutoboa.
Simba ikishinda mechi hiyo ya kimataifa itajihakikishia zaidi ya Sh800Milioni ambazo itakuwa imezipata kwa mara ya kwanza kwenye michuano hiyo ya Shirikisho miaka ya hivi karibuni.