Simba yapewa nondo nne kuiua Berkane



SIMBA ana imeanza maandalizi kamili ya kupambana na RS Berkane ya Morocco katika mchezo wao wa nne wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, lakini tajiri wao mmoja mzito ambaye aliwahi kuwapeleka katika rekodi kubwa Afrika amewapa mambo manne ambayo kama watayaweka sawa Waarabu hawatoki.

Berkane tayari wameshatua nchini jana mchana tayari kwa mchezo huo utakaopigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Benjami Mkapa, jijini Dar er Salaam na Bilionea Azim Dewji ameliambia Mwanaspoti kwamba hatua bora ya mabosi wa Simba ni kuwahi kuipanga mechi hiyo kufanyika saa 10:00 jioni.

Azim alisema kutokana na muda huo kupitishwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) hiyo ni hatua ya kwanza kubwa ambayo itawachosha Berkane ambao kwao kuna baridi.

“Kwanza nimeona mchezo utaanza saa 10 jioni hii ni hatua ya kwanza nzuri wachezaji wa Simba wanaelewa kwamba kwasasa hapa kwetu Tanzania joto ni kali lakini muda huo sio habari nzuri kwa Berkane ambao wanatoka Morocco ambako kuna baridi,” alisema Azim aliyewahi kuifadhili Simba na kufikish fainali za Kombe la CAF 1993 na kupoteza mbele ya Stella Abidjan ya Ivory Coast, rekodi ambayo hajawahi kufikiwa tena.


 
“Hata wao wakati tunacheza kule walipanga mchezo kuanza saa mbili usiku muda huo baridi inakuwa kali kidogo naamini kwa namna moja au nyingine ilisaidia kuwaondoa katika ubora wachezaji wetu.

Tajiri huyo alisema ili Simba inufaike na muda huo inatakiwa kuanza mchezo kwa kasi ili kuwachosha Berkane ambao watakuwa wanapambana kuzoea hali hiyo ya hewa kabla ya jua kupoa.

Alisema Wekundu hao wanatakiwa kucheza mpira wa kushambulia haraka kwenda golini kwa viungo wao kuharakisha wanafika golini kisha watumie kwa wingi nafasi ambazo wanatengeneza.


“Kucheza kwenye joto pekee hakutasaidia kitu, inatakiwa sasa ni kucheza soka la kwenda mbele (direct football) wafike haraka langoni mwa Berkane wakiwakimbizwa watachoka haraka hapo itakuwa ni faida kucheza katika muda huo na washambuliaji wafunge mabao.

“Kuna wale watu wa pembeni kina Banda( Peter) na yule rafiki yangu Morrison (Bernard) wanatakiwa kuwakimbiza hawa wakiwawahi watawatoa mchezoni, mabao ya mapema yanatakiwa, huwezi kutumia kila nafasi ila wasiende mapumziko bila kufunga angalau mabao mawili.

Azim aligusia ubora wa uwanjani akisema kocha wa Simba Pablo Franco anatakiwa kurekebisha makosa ya kiufundi katika upangwaji wa kikosi ambapo wengi hawakuridhika na jinsi timu ilipangwa mchezo wa ugenini.

“Simba ilicheza vizuri kule Niger, lakini Morocco haikucheza vizuri wengi tulipata wasiwasi juu ya mfumo kocha alioanza nao, ni wakati wa kusahihsiah makosa.”


 
Aliongeza pia mabeki wa kati nao wanatakiwa kucheza kwa ubora mkubwa kwa kuhakikisha wanaruka katika mipira ya juu lakini akiwatahadharisha kutozalisha mipira ya adhabu wala kukubali krosi zao zipite ndani ya eneo la hatari.

“Pia, tusiruhusu krosi wala kona wao watataka sana mashambulizi ya namna hiyo ili wanufaike, kwani ina watu warefu, hatutakiwi kufanya makosa kuwaruhusu langoni mwetu, tubaki salama.”

MSIKIE TRY AGAIN

Nao uongozi Simba umewageukia wachezaji na kuwataka wapambane, wakiiheshimu RS Berkane katika mechi yao ya Jumapili ili kujiweka pazuri kusonga mbele katika Kundi D.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema, mchezo huo ni mgumu.


Alisema, walipoteza ugenini, ila kikosi chao kina uwezo wa kufanya vizuri nyumbani kama wachezaji watatulia na kuwaheshimu wageni ndani ya dakika 90.

“Berkane ni wazuri, tunatakiwa tupambane tushinde nyumbani. Wachezaji wetu wapambane,” alisema.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad