Kiungo Mshambuliaji wa Tanzania Saimon Happygod Msuva ameitabiria makubwa Simba SC kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, baada ya kuifuatilia na kuridhishwa na uwezo wa kikosi cha Mabingwa hao wa Tanzania Bara.
Msuva ambaye kwa sasa yupo nchini kufuatia mgogoro wa kimaslahi uliopo kati yake na Uongozi wa Wydad Casablanca ya Morocco amesema ameifuatilia Simba SC tangu ilipoanza kupambana kwenye Michuano ya Kimataifa msimu huu na kuona jambo tofauti kwenye kikosi cha Mabingwa hao.
Amesema uzoefu na kujiamini kwa Benchi la Ufundi na Wachezaji wa Simba SC kutaisaidia sana klabu hiyo kwenye mapambano ya kimataifa msimu huu, hasa inapokua nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa.
“Simba SC nawaona wakifika mbali kwenye anga za kimataifa hasa kwenye mashindano haya ya kimataifa kwa sababu wana timu bora yenye uzoefu wakutoka na kujiamini.”
“Kwa mashindano ya Afrika ukiwa na uhakika wa kupata ushindi nyumbani na angalau sare ugenini, unakuwa na uhakika wa kufika mbali na Simba SC wanaweza kufanya hivyo, sina shaka nao zaidi ya kuwasihi wachezaji waendelee kupambana na kujiwekea lengo la kufika mbali.”
Simba SC inongoza Msimamo wa Kundi D ikiwa na alama 07, baada ya kuifunga RS Berkane Jumapili (Machi 13) Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es salaam, ikifuatiwa na ASEC Mimosas yenye alama 06 sawa na RS Berakane, huku Union Sportive Gendarmerie Nationale ‘USGN’ ikiburuza mkia kwa kuwa na alama 04.
Simba SC itacheza tena Jumapili (Machi 20) mjini Cotonou-Benin dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast huku RS Berkane itakaribishwa mjini Niamey katika Uwanja wa Général Seyni Kountché kucheza dhidi ya Union Sportive Gendarmerie Nationale ‘USGN’.