Kiongozi wa upinzani wa Urusi aliyefungwa jela, Alexei Navalny amechapisha jumbe kwenye mtandao wa Twitter wenye maneno makali akitoa wito wa kufanyika kwa maandamano ya kila siku nchini Urusi na kwingineko.
Navalny amekaa mwaka mmoja gerezani baada ya kunusurika shambulio la sumu ambalo anailaumu Ikulu ya Kremlin.
Mwezi uliopita alifunguliwa mashtaka mapya ambayo yanaweza kuchangia kifungo chake kuongezwa kwa zaidi ya muongo mmoja.
"Sisi - Warusi - tunataka kuwa na taifa la amani. Lakini huenda ni watu wachache wanaweza kutuita hivyo sasa," ameandika kutoka gereza lenye ulinzi mkali mashariki mwa Moscow ambako amefungwa.
Lakini Warusi wanapaswa "angalau wasiwe taifa la watu wasio na hofu" ambao "wanajifanya kuwa hawatambui vita".
"Ni muongo wa tatu wa Karne ya 21, na tunatazama habari kuhusu watu wanaochomeka kwa mabomu, nyumba zinapigwa mabomu," anasema.
"Tunatazama vitisho vya kweli vya kuanzisha vita vya nyuklia kwenye TV zetu."