Siri Wanawake wa Kimasai Kupeana Watoto



Kwa mujibu wa utafiti uliowahi kufanywa na gazeti hili la Mwananchi miaka minane iliyopita wilayani Loliondo, Wamasai wana upendo wa kimila uliopitiliza ambao hauwezi kuonekana kwa makabila mengine kwa sababu hufanyika katika mazingira ya siri ili kuzuia usumbufu na kero.

Upendo huo ni ule wa kupeana watoto. Wanawake ambao kwa bahati mbaya hawajabahatika kupata watoto hawafukuzwi kama inavyofanyika kwa makabila mengine bali hupewa watoto kwa siri makusudi kuepusha fadhaa na adha ya ugumba, tatizo ambalo husumbua ndoa nyingi.

Kutokana na utaratibu huo, kwa Wamasai hakuna mgumba. Huo ni utaratibu unaomwezesha kila mwanamke kufurahia kupakata mtoto hata kama hakuzaa.

Wanaotoa mtoto ni ndugu katika ukoo. Anaweza kuwa mtoto wa baba mkubwa, mdogo au ndugu wa tumbo moja ambao hukubaliana kumpa mtoto mwanamke ambaye imeonekana hawezi kupata mtoto.


Makabidhiano hayo huanza kufanyika mapema baada ya ndugu mmoja kushika mimba. Ukoo hukaa na kuamua kuwa mtoto atakayezaliwa atapewa mtu fulani.

Kwa kuwa hiyo ni mila yao, yule mwenye ujauzito huridhia kwa moyo wake kumpa mtoto ndugu yake, huku akila kiapo kutomdai baadaye au kutoa siri kwa mtoto atakayeaminishwa kuwa huyo ndiye mama yake halisi.

Siku za kujifungua zinapokaribia, mwanamke anayetakiwa kupewa mtoto hutakiwa kuwa karibu. Baada ya hapo mwanamke mgumba huondoka na mtoto wake, kwenda kuanza maisha mapya bila wasiwasi wowote.


Siri hii ni kubwa miongoni mwa jamii yao na wanawake wanaotoa watoto wao kuwapa ndugu au rafiki zao, hutakiwa kuitunza.

Laibon (mganga wa jadi) wa jamii ya Wamasai wa Wasso, Mkenga Kitupey, aliliambia gazeti hili kuwa wakati wa makabidhiano ya mtoto, mwanamke ambaye hajazaa hutakiwa kumpa aliyezaa ndama jike.

Mkenga alisema ndama huyo hufanyiwa dawa za kimila kama maagano kati ya wanawake hao wawili. Agano kuu ambalo wanawake hao huwekeana ni kutunza siri.

Hata ikitokea baadaye mtoto akagundua kuwa yule anayemlea si mama yake mzazi, hatakiwi kuchukua uamuzi wowote kwa sababu ya maagano ya kimila yaliyokwishafanyika.


Mtoto hatakuwa na namna ya kumuacha mama yake mlezi, kwa sababu tayari mila zimeshafanyika na pia ni dhambi kumuacha mama mgumba akiwa hana mtoto.

Katika imani za kabila la Wamasai ni nadra kuwaona watoto pacha. Ni vigumu ukawaona watoto pacha wanaotembea pamoja, kula au kwenda shule pamoja.

Si kwamba Wamasai hawazai pacha, bali kiimani ni mwiko pacha kulelewa katika nyumba moja.

Zamani ilionekana ni mkosi mwanamke kuzaa watoto wawili, kwani lilionekana siyo jambo la kawaida kwa jamii hiyo, hivyo pacha mmoja alipelekwa katika familia nyingine. Ingawa yapo mengi yaliyotajwa kiimani kuhusu pacha, jambo la msingi ni kuwa wazee walidhani mapacha hawawezi kukua vizuri katika familia moja.


Walidhani mapacha wakilelewa na mama mmoja hawatapata malezi mazuri na hivyo hawatakua vizuri na ndiyo maana ilionekana bora watenganishwe, mwingine akalelewe kwingine.

Mila mtoto akizaliwa

Mtoto wa Kimasai anapozaliwa hapewi jina rasmi, bali hupewa jina la muda lijulikanalo kama ‘embolet’, ikiwa na maana ya kufungua.

Kuanzia siku ya kuzaliwa, hadi siku ya sherehe ya kumtaja mtoto, atatambuliwa kwa jina la embolet. Watoto wa Kimasai hutofautiana kiumri wakati sherehe ya kuwapa majina inapofanyika.

Kulingana na nasaba ya familia zao, baadhi yao wanaweza kuwa na umri wa miaka mitatu kabla ya kufanyika kwa sherehe ya majina ya watoto wa Kimasai, inayojulikana kama ‘Enkipukonoto Eji’ ikimaanisha kutoka kifungoni au kutoka katika hali ya kutengwa. Katika maandalizi ya sherehe za Enkipukonoto Eaji, mama na mtoto hukaa tu ndani na kuacha nywele zikue zaidi.

Maandalizi ya sherehe za majina ya watoto wa Kimasai huchukua hadi siku mbili na huhusisha shughuli mbalimbali.


Walezi au wafadhili wawili wa kwanza, mmoja wa mama na mwingine wa mtoto wa Kimasai, huchaguliwa wakati wa sherehe hizo. Kila mfadhili lazima awe katika kikundi cha umri sawa na mama au mtoto na abaki na uhusiano wa karibu na familia. Kisha kondoo dume wawili huchaguliwa, mmoja wao huchinjwa na kutumiwa kama kitoweo wakati wa sikukuu.

Ni wanawake pekee wanaoruhusiwa kula nyama ya kondoo huyo.

Hii inafanywa ili kuwafurahisha wanawake na kujaribu kufidia uchungu wanaohisi wakati wa kujifungua.

Wanawake pia hula nyama kama njia ya kumshukuru Engai, hili ni neno la Kimasai linalomaanisha ‘Mungu’, au ‘Aliye Mkuu’, kwa kuwapa uwezo wa kuzaa watoto.

Kisha kwenye mkono wa kuume wa mtoto mama huweka Olkererreti, ambayo ni bangili iliyotengenezwa kutokana na mguu wa kulia wa kondoo.

Kisha kibuyu maalumu cha Kimasai hutumika kuteka maji mtoni. Mama anakunywa maji haya wakati sherehe ya kuwapa watoto majina inapoanza.

Wakati nyama iko tayari na shughuli zote zilizoorodheshwa zimekamilika, mama hupewa maji anywe, na mfadhili wa mama anatangaza kwamba sherehe imeanza.

Wanawake wengine huishi pamoja na mama na mfadhili wake, kisha huanza kutathmini ‘embolet’ ya mtoto na kuamua jina lake jipya kulingana na utu wa mtoto tangu kuzaliwa.

Ikiwa watu wengi wanapenda jina lake la muda, kuna uwezekano wa kuendelea kutumika kwa jina hilo.

Wanawake humbariki mtoto kwa jina lake jipya kwa kumwambia mtoto huyo kwamba “Jina hili linaishi ndani yako” na jina hilo jipya, linalojulikana kama ‘enkama enchorio’, ni la kudumu.

Hatimaye, mama huondoa bangili ya mtoto na sherehe inakuwa imefika mwisho.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad