MFUMO wa ulinzi wa anga la NATO wa Patriot umeanza kuwasili Slovakia na unatazamiwa kuendelea katika siku zijazo, Waziri wa Ulinzi wa Slovakia Jaroslav Nad amesema.
Mfumo huo ulioundwa na Marekani umesafirishwa hadi nchini humo kama sehemu ya jitihada za NATO kuimarisha ulinzi wa nchi wanachama wa Ulaya Mashariki ili kukabiliana na operesheni ya kijeshi ya Urusi nchini Ukraine.
Slovakia, ambayo ni sehemu ya NATO na EU, ina wakazi milioni 5.5 na inashiriki mpaka wa urefu wa kilomita 100 na Ukraine.
"Mfumo huo utawekwa kwa muda katika kituo cha jeshi la anga la Sliac. Maeneo zaidi ya kupelekwa mfumo huo yanazingatiwa ... kwa hivyo mwavuli wa usalama unashughulikia sehemu kubwa zaidi inavyowezekana ya eneo la Slovakia," Nad aliandika katika ukurasa wake wa Facebook.
Mfumo wa Patriot ulitolewa kwa Bratislava na wanachama wenzake wa NATO, Ujerumani na Uholanzi, utahudumiwa na wanajeshi kutoka nchi hizo. Kikundi cha vita cha kambi hiyo nchini Slovakia kinatarajiwa kuwa na wanajeshi 2,100.
Waziri huyo alisema Patriot haitachukua nafasi ya S-300 ya wakati wa Soviet ya Slovakia, lakini badala yake itatumika kama nyenzo ya ziada ya ulinzi wa anga wa nchi hiyo. Hata hivyo, alikariri nia ya Bratislava kupeleka mfumo mwingine kwa sababu ya "umri, hali ya kiufundi, [na] uwezo duni" wa S-300 na kwa sababu mzozo wa Ukraine umefanya ushirikiano wa kijeshi na Urusi "kutokubalika."