SPIKA wa Bunge la Tanzania, Dk. Tulia Ackson, amesema katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, nchi imepiga hatua kwenye masuala ya demokrasia. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).
Spika Tulia ametoa kauli hiyo leo Jumamosi, tarehe 19 Machi 2022, akifungua kongamano la tathmini ya mwaka mmoja wa Rais Samia madarakani, lililofanyika kwenye Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), jijini Dodoma.
Spika Tulia amesema, kuimarika kwa demokrasia kunathibitishwa na kitendo cha Mwenyekiti wa Chama cha ADC Taifa, Hamad Rashid, kushiriki kongamano hilo.
“Hapa mmemuona mzee wetu Hamad Rashid, kitendo cha yeye kuwepo hapa kuja kufanya tathmini ya mwaka mmoja wa Rais Samia, kunaashiria kwamba nchi yetu kidemokrasia tumepiga hatua, tunaweza kukaa pamoja namna hii, tukajadiliana pamoja na tofauti zetu za vyama, tunapiga hatua ndani na nje ya nchi,” amesema Spika Tulia.
Aidha, Spika Tulia amesema Rais Samia amefanikiwa kuimarisha demokrasia ya kiuchumi, kwa kufanya ziara katika mataifa ya nje.
“Kwenye eneo la uwekezaji na kukua kwa demokrasia kumesaidia hata demokrasia ya uchumi. Nyie mmeona akizunguka kwenye mataifa mbalimbali kutafuta fursa ambazo zinalifanya Taifa letu lipige hatua. Sasa hatua tunapiga sio tu Taifa letu kwa upande wa maendeleo,” amesema Spika Tulia.