Steve Nyerere akubali yaishe
MSANII wa vichekesho nchini, Steven Mengele ‘Steve Nyerere’, amesema amepokea uamuzi wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kumwambia asitekeleze majukumu yake katika Shirikisho la Muziki Tanzania (Shimuta), hadi itakapoamriwa vinginevyo.
Jana Basata ilimsimamisha Steve Nyerere, asianze majukumu yake ya usemaji wa Shimuta, hadi itakapotolewa uamuzi mwingine na baraza hilo kutokana na kuwepo mzozo, kati ya viongozi wa Shimuta na baadhi ya wasanii wanaopinga uteuzi wa msanii huyo.
Katika taarifa yake ya jana, Basata ilisema ilitoa uamuzi huo baada ya kusikiliza pande zote mbili za uongozi wa juu uliomteua Steve na wajumbe wanaopinga uteuzi huo katika kikao kilichofanyika kwenye ofisi za baraza hilo, kilichokuwa na lengo la kuangalia kiini cha mgogoro huo, ili kutafuta ufumbuzi.
Basata ilifafanua kuwa ilichukua uamuzi huo kwa mujibu wa vifungu 4(1), (i) na (p) na 4A vya Sheria (Sura 204) vikisomwa kwa pamoja na Kanuni ya 19 ya Kanuni za Baraza (G.N 43/2018), limepewa mamlaka ya kusajili na kusuluhisha migogoro ya wasajiliwa wake, yakiwemo mashirikisho ya sanaa nchini.
Akizungumza na Daily News Digital jijini Dar es Salaam leo, Steven Nyerere amesema, baadhi ya wanaomkataa ni watu wenye tabia mbaya na roho mbaya, wasiopenda maendeleo, lakini kwa vile kuna tamko la Basata, basi kwa sasa hana cha kufanya zaidi ya kusubiri maelekezo mengine.
"Haiwezekani kupendwa na wote, dhahabu ili ing’ae lazima ipite kwenye moto, Steve ni dhahabu.
"Shirikisho lipo muda mrefu, lakini baada ya kumtaja Steven Nyerere yameibuka mengi, kila mtu analijua shirikisho. Hivi sasa nasubiri maelekezo ya Basata, mtu mzima dawa na Mungu yupo," amesema Steve Nyerere.