Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikiwa na hifadhi kubwa ya gesi asilia, bado imeendelea kupambana kupata nishati ya mafuta ya kuendeshea vyombo vya usafiri na viwandani.
Tanzania inakadiriwa kuwa na mita trilioni 230 za ujazo za gesi asilia, ingawa zilizothibitishwa mpaka sasa ni futi trilioni 57.5, hivyo kuiweka kwenye ramani ya dunia ikishika nafasi ya 82.
Gesi hiyo tayari imeanza kuchimbwa katika visiwa vya Songosongo wilayani Kilwa, mkoani Pwani na eneo la Msimbati mkoani Mtwara, ikitumika kuzalisha umeme na kuendesha mitambo ya baadhi ya viwanda nchini.
Pamoja na wingi wa hazina ya gesi hii muhimu, kwa kiasi kikubwa Tanzania bado inategemea mafuta kuendesha mitambo ya viwanda vyake pamoja na magari ya mizigo na abiria na pia baadhi ya majenereta ya kuzalisha umeme unaosambazwa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Uhalisia wa hali ukiwa hivyo, Shirika la Petroli Tanzania (TPDC) kwa upande wake lina mkakati wa kuanzisha vituo vya kuweka gesi kwenye magari yaliyoongezewa mfumo unaotumia nishati hiyo.
Ni gesi hiyo inayoelezwa na wadau kuwa ndiyo suluhisho la tatizo la mafuta nchini.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika kitaifa visiwani Zanzibar juzi, Rais Samia Suluhu Hassan alisema bei ya mafuta inaathiriwa vita vya Russia na Ukraine vinavyoendelea.
“Mafuta yanapanda mno bei na jinsi yanavyopanda, Tanzania hatutanusurika. Bidhaa zote zitapanda bei, nauli zitapanda, kila kitu kitapanda bei. Thamani ya kila kitu itapanda bei kwa sababu mafuta yamepanda,” alisema Rais Samia.
Mkakati wa TPDC
Julai 2020, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, James Mataragio alisema Sh28 bilioni zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya kujaza gesi kwenye magari ambavyo vilitarajiwa kukamilikia Julai 2021, lakini baadaye akasema janga la Uviko-19 limesababisha vichelewe.
Januari 2021, Mkurugenzi wa Biashara ya Mafuta na Gesi wa TPDC, Dk Wellington Hudson aliliambia Mwananchi kuwa hadi Desemba 2020 shirika lilikuwa limekamilisha usanifu na michoro ya kihandisi na kufanya tathmini ya athari za mazingira.
“Kwa sasa, shirika lipo katika hatua za mwisho za maandalizi ya kumpata mkandarasi wa kutekeleza miradi hii. Inatazamiwa ujenzi utaanza Aprili 2021 na utakamilika ndani ya miezi minane. Gharama za mradi zitajulikana pindi mkandarasi atakapopatikana,” alisema.
Miezi minane aliyosema Dk Hudson ilikamilika Desemba 2021 na mpaka sasa bado kuna kituo kimoja tu cha kujazia gesi kilichopo Ubungo, kwani vilivyotarajiwa havijajengwa.
Alipowasilisha bajeti ya Wizara ya Nishati ya mwaka 2021/22, aliyekuwa Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani alisema ujenzi wa vituo vya kushindilia gesi asilia (Compressed Natural Gas (CNG)) katika Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani utasaidia kuongeza matumizi ya gesi asili kwenye magari.
Vituo vya CNG vilitarajiwa kutajengwa katika kituo cha mabasi yaendayo haraka kilichopo Ubungo, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na pembezoni mwa Barabara ya Sam Nujoma na vituo vidogo vya kupokelea na kusambaza gesi asilia vingejengwa Soko la Samaki Feri, Hospitali ya Taifa Muhimbili na katika kiwanda cha dawa cha Kampuni ya Kairuki Pharmaceutical kilichopo Zegeleni mjini Kibaha.
Dk Kalemani alisema katika mwaka wa fedha 2020/21, kazi iliyofanyika ilikuwa kutangaza zabuni kumpata mkandarasi wa vituo vitano vya CNG baada ya kukamilika kwa kituo cha Ubungo ambako jumla ya magari 250 yaliwekewa mfumo wa gesi asilia, hivyo kufikisha zaidi ya magari 700 yanayokitumia.
Juni 26 mwaka jana alipozindua gari linalotumia gesi, Dk Kalemani alisema vituo hivyo vitano vinajengwa na tayari viwili vya kuwekea gesi vinatoa huduma, yaani cha Ubungo na chuo kikuu.
“Tumetoa maelekezo kwa wataalamu wetu, mwakani tutaweka vituo kwa kila jiji kujaza gesi katika magari, tunaanza na Dodoma, Mbeya, Tanga na Arusha na tutakuwa na vituo vidogovidogo. Tunataka tuwe na vituo vya kujazia gesi sawa na vituo vya mafuta,” alisema.
Kituo cha kwanza cha gesi kilichopo Ubungo Maziwa kilichojengwa mwaka 2009 kinamilikiwa kwa ubia TPDC na Kampuni ya Panafrican Energy (PAET).
Juzi, Waziri wa Nishati, Januari Makamba alisema kutokana na ongezeko la bei ya mafuta duniani, matumizi ya gesi kwenye magari ni fursa nzuri, lakini changamoto ni uhaba wa miundombinu.
“Ilikuwa ni rahisi hata kuweka mkakati wa kitaifa kuhakikisha magari mengi yanayoingizwa nchini yanatumia gesi, lakini si jambo rahisi kwa kuwa vituo vya kujazia gesi ni vichache,” alisema.
Hata hivyo, Serikali inahimiza mashirika ya umma, kampuni binafsi na taasisi za Serikali kutumia gesi.
Msemaji wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Mustafa Mwalongo alisema wengi hawajafikiria kubadilisha mfumo wa magari yao ili yatumie gesi wala kununua magari yenye mfumo huo kwa kuwa hawana uelewa nayo.
“Hatujawahi kufikiri kuwa na mabasi yanayotumia gesi kwa kuwa teknolojia hiyo ni ngeni kwetu, haijawahi kutokea mtu mwenye ufahamu akatueleza kuhusu hilo wala kuyaona mabasi yanayotumia nishati hiyo hata nchi jirani, labda tujifunze,” alisema Mwalongo.
Msemaji huyo alisema basi ni usafiri unaohudumia wengi, hivyo wanaogopa kuingia kwenye jambo wasilojua changamoto zake.
Mpaka sasa kuna karakana mbili zinazotumika kuweka mifumo ya CNG kwenye magari ambazo ni ya Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na ya Kampuni ya BQ Contractors.
Ujenzi wa vituo vitano
Dk Hudson alisema usanifu wa mradi wa gesi iliyoshindiliwa kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwamo kwenye magari umekamilika.
“Tathmini ya athari ya mazingira na jamii imekamilika kwa zaidi ya asilimia 90. Mradi huu sasa upo katika hatua ya kumtafuta mkandarasi, tayari zabuni ilishatangazwa na tunapokea maombi kutoka kwa makandarasi mbalimbali,” alisema.
Alisema shirika linakamilisha upitiaji maombi ya makandarasi ili kumpata mshindi atakayejenga mradi huo.
“Inategemewa mradi utachukua miezi minane kukamilika tangu siku ya kusainiwa kwa mkataba,” alisema Dk Hudson.
Kuhusu kuchelewa kwa mradi, alisema kumetokana na kurudiwa kwa tangazo la zabuni ya kumpata mkandarasi baada ya kushindwa kupatikana mara ya kwanza kutokana na walioomba kukosa vigezo.
Dk Hudson alisema TPDC inatambua fursa ya kutumia gesi kwenye magari na tayari wananchi wengi wamehamasika kuitumia gesi asilia kwenye magari yao, zikiwamo daladala na malori.
“Hii inatokana na ukweli kwamba gesi ni nafuu sana ukiilinganisha na petroli au dizeli,” alisema.
Kuhusu kuongeza vituo zaidi kama mbadala wa mafuta, alisema utekelezaji utaanza na ujenzi wa vituo vitano, lakini Serikali inakusudia kuwekeza zaidi kwa kujenga vingi zaidi kurahisisha upatikanaji wake nchini.
“Sambamba na jitihada hizi, Serikali imeziruhusu kampuni binafsi kuwekeza katika ujenzi na uendeshaji wa vituo vya kujaza gesi kwenye magari. Hadi sasa kampuni 11 zimeruhusiwa kufanya biashara hii, zinakamilisha utaratibu wa kupata leseni kutoka Ewura (Wakala wa Udhibiti wa Nishati na Maji),” alisema Dk Hudson.
Faida za gesi dhidi ya mafuta
Taarifa zinaonyesha matumizi ya gesi asilia ni nafuu ikilinganishwa na dizeli au petroli, kwani hupunguza gharama kwa takriban asilimia 50. Kilo moja ya gesi hiyo kwa sasa ni Sh1,550 wakati lita moja ya petroli ni Sh2,540 kwa bei ya jijini Dar es Salaam.
Ukiacha gharama za ununuzi wa nishati hiyo, kilo moja ya gesi huweza kwenda umbali sawa na mara moja na nusu ya unaotumiwa na lita moja ya mafuta. Hata kulihudumia gari, linalotumia gesi hupelekwa matengenezo baada ya kwenda umbali mara mbili ya uliotembea gari linalotumia mafuta.
Hii ina maana kama gari linatembea kilomita 10 kwa lita moja ya mafuta basi kwa gesi litatembea kilomita 15 kwa kilo moja na kama ilikuwa linafanyiwa matengenezo baada ya kilomita 3,000 sasa itakuwa baada ya kilomita 6,000.
Gharama ya kubadilisha mfumo kuliwezesha gari kutumia gesi ni wastani wa Sh1.5 milioni kwa gari lenye silinda tatu, Sh1.85 milioni kwa lenye silinda nne, Sh2.35 milioni kwa lenye silinda sita na Sh2.7 millioni kwa silinda nane.
Lakini gharama hiyo inaweza kuwa kubwa kwa magari yanayotumia injini za dizeli kwa kuwa mifumo yake ni ghali kwani lori (semi trailer) gharama yake ni Sh19.4 millioni na basi kubwa ni Sh22.3 millioni.
Gesi asilia inayozalishwa nchini itawasaidia watumiaji wa nishati hii kuwa na uhakika wa kuendesha magari yao wakati wote kwa bei inayotabirika zaidi kuliko ilivyo kwa kutumia mafuta kutoka nje ya nchi ambayo bei yake hubadilika kutegemea mwenendo wa soko la dunia.
Matumizi ya gesi asilia kwenye magari yatasaidia kuokoa fedha za kigeni ambazo zingetumika kuagiza dizeli na petroli kutoka nje.
Vilevile gesi asilia ni nishati rafiki kwa mazingira kwa sababu inatoa kiwango kidogo cha gesi ya ukaa ikilinganishwa na petroli na diseli hivyo kupunguza uchafuzi wa mazingira.
Mwenendo wa bei ya mafuta duniani
Mpaka jana bei ya pipa moja la mafuta katika soko la dunia ilifika dola 126 za Marekani (Sh291,689), kubwa zaidi kwa miaka ya hivi karibuni. Kwa mara ya mwisho bei kama hiyo ilishuhudiwa mwaka 2008 pipa moja lilipouzwa dola 130. Mwaka huu, wachambuzi wanasema bei inaweza kufika dola 150 kwa pipa moja.
Februari 19 bei ilipokuwa inaanza kupanda, Waziri Makamba alisema Serikali inafuatilia na itachukua hatua muhimu ya kuunusuru uchumi endapo hali italazimu.
“Hali inashtua, lakini njia zote za kudhibiti zipo wazi, Tanzania kwa siku tunatumia lita milioni 10, ni bidhaa nyeti lakini kwa sasa tunaweza kumudu gharama iliyopo, tunaendelea kufuatilia ikifikia dola 100 kwa lita tutachukua hatua zaidi, ikiwezekana hata kugusa tozo zilizowekewa uzio,” alisema.
Kutokana na mwenendo wa bei ya mafuta duniani, Februari 28 Serikali iliondoa tozo ya Sh100 katika kila lita moja kwa miezi mitatu mpaka mwishoni mwa Mei ili kutoa unafuu kwa watumiaji.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Nishati kuhusu punguzo hilo ilieleza ni uamuzi unaotokana na kupanda kwa bei za mafuta.
“Katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali imeondoa Sh100 kwa kila lita moja ya dizeli, petroli na mafuta ya taa zilizopaswa kulipwa na watumiaji wa mafuta nchini kwa muda wa miezi mitatu kuanzia Machi hadi Mei huku tukiendelea kutathmini mwenendo wa bei katika soko la dunia,’’ ilisema.