SHIRIKA la Umeme (TANESCO) limesema kuanzia Julai mwaka huu litakuwa na mfumo wa ununuzi wa umeme ambao utawezesha wateja wao kuweka umeme kwenye mita papo hapo (automatically) tofauti na wa sasa unaohitajika ‘token’ kuingizwa kwenye mita zao.
Mkurugenzi wa TEHAMA wa shirika hilo, Cliff Maregeli, alibainisha hayo jana alipozungumza na Nipashe kuhusu mfumo huo unaotarajiwa kuanza na majaribio kwa kubadili mita na kuweka mpya zenye uwezo wa kusoma mfumo wa TANESCO.
Maregeli alisema kwamba mita zilizopo sasa hazina mfumo wa kisasa kubaini masuala mbalimbali ikiwamo eneo ambako umeme umekatika au mteja amekosa huduma kutokana na kuchelewa kulipia huduma.
“Mita tulizonazo sasa hivi hazina uwezo wa kuongea na mifumo ya TANESCO. Sasa ukinunua umeme utahitajika kutafuta njia ya kuufikisha umeme nyumbani kwako. Tunakuja na njia ambayo tumeweka, tukikupa wewe inajua hiyo token ni ya kwetu.
“Sasa hivi shirika linakuja na mfumo wa mitajanja, tutaweza kufanya vitu vingi katika mfumo huu, utaweza kununua umeme wa shilingi 2,000 na ‘automatically’ (moja kwa moja) utaingia kwako,” alisema Maregeli.
Alibainisha kuwa mradi huo upo kwenye hatua ya kukamilishwa na utaanza kwa majaribio kwenye maeneo yaliyo na watumiaji wengi wa huduma hiyo.
"Tutachagua eneo kama sehemu ya majaribio kwa kubadili mita zote na wateja waanze kutumia mfumo huu. Eneo kamili utaanzia wapi bado haijapangwa lakini miradi mingi ya aina hii huanzia kuliko na wateja wengi wa TANESCO, mfano Dar es Salaam," alisema.
TANESCO ni shirika la umma lililoanzishwa mwaka 1964 likiwa chini ya usimamizi wa wizara yenye dhamana ya nishati nchini.