Tanzania inatenga vitalu vya kuwinda wanyamapori kwa njia ya mnada ili kuongeza mapato zaidi, ambapo inalenga kukusanya TZS bilioni 69.6 kutokana na mnada huo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro amesema wawindaji watakaofanikiwa wataruhusiwa kuua Tembo, Simba na wanyama wengine wakubwa wanaoonekana kutokuwa na tija.
Takribani 25% ya mapato yatatumika kusaidia jamii zinazoishi karibu na vitalu vya uwindaji.
Mengine yatatumika kwenye programu za kupambana na ujangili, doria za wanyamapori, usafiri, ufuatiliaji na kuwafungulia mashtaka wahalifu.
Mapato kutoka kwa wanyamapori yalipungua kutoka TZS bilioni 111 mwaka wa 2019 hadi TZS bilioni 44 mwaka jana kutokana na janga la UVIKO19.
Tanzania ni nchi inayoongoza barani Afrika kwa uwindaji mkubwa wa wanyama katika maeneo yasiyo na uzio. Ina takribani nusu ya idadi ya simba-mwitu duniani na ya tatu kwa kuwa na idadi kubwa ya tembo Afrika.
Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Mazingira (IUCN) ya mwaka 2019, asilimia 72 ya maeneo makubwa ya uwindaji nchini Tanzania sasa yameainishwa kuwa yamepungua, kwa sababu wanyama wakubwa walikuwa wamewindwa kutoka katika maeneo hayo.