SIMBA inazidi kupasua anga kimataifa ambapo sasa wanahitaji ushindi katika mechi moja tu kati ya mbili walizobakiza kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho ili watinge hatua ya robo fainali.
Lakini wakati wakiendelea kupambana kuiletea heshima nchi kimataifa, vigogo wa timu hiyo kwa kushirikiana na benchi la ufundi, wameshaanza mikakati mizito ya kuimarisha kikosi chao msimu ujao na wamepanga kutumia kipindi hiki kutazama mastaa ambao wataifanya iwe tishio msimu ujao.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ amelidokeza Mwanaspoti kuwa wamepanga kufanya usajili wa kishindo ambao utakuwa wa wachezaji wanne wa kimataifa katika dirisha kubwa la usajili ambao wataimarisha maradufu kikosi chao.
Try Again ambaye anakumbukwa kwa kupeleka kilio Yanga kwa kumtwaa aliyekuwa nyota wao kipenzi, Haruna Niyonzima mwaka 2017 alisema watasajili wanne tu wa kimataifa ambao ni wachezaji wenye majina makubwa na walio na uzoefu wa kutosha wa mashindano ya kimataifa na soka la Afrika kiujumla.
“Simba huwa hatufanyi mambo kwa kubahatisha na kupiga kelele kama wengine. Sisi tunasajili wachezaji wa daraja la juu ambao wataifanya timu iwe imara zaidi,” alitamba licha ya kutotaka kuweka wazi majina na nchi za wachezaji hao kwa madai kwamba watauza mbinu za kivita lakini yajayo yanafurahisha.
Mpango wetu katika dirisha lijalo, tutasajili wachezaji wanne wa daraja la juu wa kimataifa ambao ni mastraika wawili, winga mmoja na beki wa kati mmoja. Ni wachezaji hasa na watakuwa na mchango mkubwa kwa timu,” alisema Try Again ambaye amekuwa ndani ya uongozi wa Simba miaka mingi.
Mwanaspoti lina uhakika kuwa miongoni mwa nyota hao wanne ambao Simba itawasajili yumo winga wa US Gendarmerie, Victorien Adebayor na mshambuliaji wa Zanaco ya Zambia, Moses Phiri.
Simba, hadi wakati Gendarmerie itakapokuja kuumana nao katika mechi ya mwisho ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, Adebayor atakuwa rasmi ni mwekundu wa Msimbazi wakati suala la usajili wa Phiri lilishakamilishwa tangu Januari.
Pia Mwanaspoti limedokezwa kuwa Simba ina mpango wa kuchomoa beki wa kati kutoka klabu mojawapo inayoshiriki hatua ya makundi ya mashindano ya klabu Afrika ingawa jina lake halijawekwa wazi.
Uongozi wa Simba umekoshwa na kiwango bora cha timu hiyo kwenye Kombe la Shirikisho Afrika na unaamini itafanya vizuri zaidi.
“Simba ni timu kubwa na hilo linajidhihirisha hivi sasa. Tumebakiza mechi mbili za hatua ya makundi na uongozi umejipanga vyema kuhakikisha tunapata ushindi katika michezo hiyo yote ili tumalize tukiwa tunaongoza kundi,” alisema Try Again.