SIMBA imerudi kileleni katika msimamo wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiongoza kundi D baada ya juzi kuichapa RS Berkane ya Morocco kwa bao 1-0 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Mkapa.
Matokeo hayo yameifanya Simba kufikisha pointi saba ikishinda mechi mbili, sare moja na kipigo kimoja huku nyuma yake ikiwapo Asec Mimosas ambayo juzi iliwachapa US Gendarmerie kwa mabao 2-1.
Ushindi wa Simba umekamilisha hesabu za wawakilishi hao pekee wa Tanzania katika mashindano ya Caf kwa sasa baada ya kuonekana kujipanga vyema dhidi ya RS Berkane. Mwanaspoti linakuangazia kilichojiri katika mchezo huo ulioshuhudiwa na mashabiki 35,000.
TSHABALALA MOTO
Katika matokeo ya Simba wapo wachezaji wengi wanapaswa kusifiwa, lakini staa wa kwanza kando ya mfungaji wa bao pekee atabaki kuwa nahodha msaidizi, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye mapema tu aliwatibulia wageni na kuwafichia mtu wao muhimu mwenye kasi.
Tshabalala aliwalazimisha RS Berkane kumtoa winga Tuisila Kisinda ambaye alidhibitiwa mbio zake na hakuwa na lingine uwanjani badala yake akatolewa na kuvuruga hesabu za timu yake.
Si hilo tu, Tshabalala alikuwa bora katika kupandisha mashambulizi na kuzima mashambulizi mengine ya wapinzani wao na kuifanya safu ya ulinzi Msimbazi kuwa katika ubora wake.
SAKHO BALAA
Staa aliyefunga bao pekee la mechi, Pape Sakho, anakuwa ameifungia Simba bao la pili katika mechi mbili mfululizo nyumbani za mashindano hayo. Katika mchezo dhidi ya Asec Mimosas alifunga moja ya mabao matatu.
Ukiangalia utulivu wake juzi aliwatingisha mabeki wa RS Berkane akasogea hadi ndani ya eneo la hatari kisha akafunga bao kwa utulivu akiwa katikati ya watu sita wa timu hiyo pinzani.
Sakho hajafunga bao lolote ugenini akiwa na Simba katika mashindano ya Caf, lakini anaonekana hatari anapokuwa Uwanja wa Mkapa.
KULIKONI KIBU?
Mashabiki wa Simba walitofautiana na kocha Pablo Franco kumuanzisha mshambuliaji Kibu Dennis kwani hakuwa na ubora alipokuwa anapandisha mashambulizi katika nafasi tano ambazo alipata.
Hata hivyo, Pablo anaamini Kibu alikuwa na kazi bora kutokana na kuifanya beki ya pembeni ya Berkane kutopanda juu akidai jamaa alifanya kazi bora katika muda aliokuwa uwanjani.
Wakati Pablo akitetea hilo, alitakiwa kuelewa nafasi ambazo Kibu alipata kama angetua zingeipunguzia presha Simba ambayo ushindi wa bao moja uliifanya RS Berkane kuzidisha hesabu za kutafuta bao la kusawazisha.
Kama Simba ingepata bao lingine au mengine yangeipunguza kasi au kuizima kabisa RS Berkane na hatua ambayo ingewapa utulivu wa mchezo Wekundu hao na ubora wa Peter Banda na Bernard Morrison walipoingia ulithibitisha hilo kwa Simba kuchangamka eneo la mbele.
UKUTA SIMBA FRESHI
RS Berkane ilionekana kubadilika hasa kipindi cha pili ilipokuja juu na kutishia usalama wa bao la Simba, lakini ubora wa mabeki wa wenyeji na hata viungo wakabaji ulikuwa ni kitu kilichostahili kupongezwa kwani walionekana kujipanga vyema kuzima mashambulizi.
PABLO, IBENGE HAWA HAPA
Akizungumzia mchezo huo, Pablo alisema walikuwa bora uwanjani na walitengeneza nafasi za kutosha ambazo ziliwapa ushindi muhimu kabla ya kuwafuata ugenini Asec Mimosas mchezo ujao.
“Tulitengeneza nafasi za kutosha na kucheza kwa kujipanga hatua ambayo imetupa pointi tatu muhimu tukiwa mbele ya mashabiki wetu. Huu ni ushindi muhimu kabla ya kuelekea ugenini kwenye mchezo ujao dhidi ya Asec,” alisema Pablo.
Kocha wa RS Berkane, Florent Ibenge ambaye alipoteza mechi yake ya tatu dhidi ya Simba katika Uwanja wa Mkapa akiwa na klabu mbili tofauti, alisema anaendelea kuteswa na Simba yenye ubora ingawa mchezo wa juzi ulikuwa na udhaifu flani upande wa waamuzi.
“Tunatakiwa kuutanguliza mchezo wa kiungwana (fair play). Kwa hili tuwapongeze Simba kwa kushinda, hii ni moja kati ya timu nzuri ambayo imetufunga, lakini tulijiandaa kucheza mechi ngumu ili tupate ushindi, bahati mbaya hatujakutana na waamuzi bora katika mchezo huu,” alisema Ibenge.
“Bado tuna nafasi ya kuhakikisha tunapata alama tutakapowafuata Gendarmerie kabla ya kwenda kumalizia mechi nyumbani, jambo ambalo limekuwa likituumiza ni hali ya majeruhi katika kikosi.”