Dar es Salaam. Wakati Watanzania wakishiriki maadhimisho ya kukabiliana na ugonjwa wa figo duniani jana, takwimu za Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) zinaonyesha kupokea maombi ya wananchi 36 wakiuliza uwezekano wa kuuza figo zao, sababu ikiwa ni ugumu wa maisha.
Hata hivyo, Tanzania bado haijaandaa sheria inayohalalisha mwananchi kuuza sehemu ya kiungo chake cha mwili licha ya kuwapo mijadala mara kadhaa katika jamii na ndani ya mhimili wa kutunga sheria.
Halid Mahenga, Ofisa ustawi wa Jamii kutoka Kitengo cha Figo katika hospitali hiyo, hivi karibuni alinukuliwa akisema kati ya Januari hadi Februari mwaka huu watu sita walikwenda katika hospitali hiyo kwa ajili ya kuulizia uwezekano wa kuuza figo zao.
Katika taarifa yake kwa umma, Mahenga alisema mwaka 2021, idara hiyo ilipokea maombi 27 na kati ya mwaka 2019 na 2020, kulikuwa na watatu waliohitaji kujua utaratibu wa kuuza figo zao katika hospitali.
Katika mahojiano na gazeti dada la The Citizen, Dk Jonathan Mngumi alisema baadhi ya sababu walizoeleza katika maombi yao ni changamoto za ugumu wa maisha.
“Hatufanyi biashara, haiwezekani kwa sababu zozote zile ukahitaji kuuza figo yako, ni kinyume cha sheria,” alisema Dk Mngumi.
“Ni muhimu watu wakatambua kwamba ni makosa kisheria, mgonjwa akihitaji upandikizaji, hospitali itazingatia kanuni zinazohitajika kwa mtu anayetakiwa kuchangia figo kwa mgonjwa fulani mwenye uhusiano wa damu,” alisema Mahenga.
Alisema wakati Serikali ikiendelea kufanyia kazi maandalizi ya sheria ya upandikizaji wa viungo, hospitali hiyo kwa sasa inaendelea kuzingatia misingi yote ya maadili kitaaluma katika upandikizaji wa figo.
Idadi ya vifo inaendelea kutengeneza wasiwasi baada ya Mratibu wa huduma za figo nchini, Dk Linda Ezekiel kudai watu milioni 1.2 duniani walifariki dunia kwa sababu ya figo kushindwa kufanya kazi mwaka 2015, huku milioni 7.1 wakikosa huduma ya usafishaji damu ‘dialysis’ mwaka 2010.
“Asilimia 98 ya wagonjwa wanaohudhuria kliniki za kisukari Mwanza wana ugonjwa sugu wa figo na Tanzania ina takribani watu 5,800 mpaka 8,400 ambao wanahitaji huduma ya dialysis, lakini ni wagonjwa 2,750 tu wanaopata huduma hiyo kwa sasa,” alisema.
Dk Linda alitaja vyanzo vikuu vya ugonjwa sugu wa figo kuwa ni shinikizo la juu la damu, kisukari na maambukizi.
Alisema kwa sasa nchini kuna madaktari bingwa wa figo 25, wauguzi bingwa 250, vituo vya mafunzo sita, vituo vya kupandikiza figo viwili vilivyopandikiza wagonjwa 93, huku kukiwa na vituo vya huduma za usafishaji damu vya umma 12 na binafsi 38 vinavyotoa huduma kwa wagonjwa 2,750.
Daktari bingwa mshauri wa magonjwa ya figo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) iliyopo Dodoma, Kessy Shija alisema: “Figo huumia kidogo kidogo na bahati mbaya maumivu ya kwenye figo huwezi kuyatambua mpaka utakapofika hatua ya mwili kushindwa kuchuja taka mwili.
“Tatizo la kufeli kwa ghafla hutokea iwapo mtu amepata ajali na kumwaga damu nyingi, figo huchuja damu isipopata damu ya kutosha, inaweza ikaumia au kupoteza maji mengi kwa kuharisha au kutapika, hiyo ni mshtuko yaani ghafla,” alisema.
Dk Kessy ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Figo BMH alisema Tanzania kuna tafiti chache zimefanywa na ukubwa wa tatizo umeonekana kwa asilimia 7 mkoani Kilimanjaro na asilimia 15 Kisarawe, lakini hiyo ni nje ya hospitali zinazotoa huduma ya magonjwa ya figo kuanzia waliolazwa au kuhudhuria kliniki.
Matibabu, kujikinga
Dk Kessy alisema kwa Afrika chanzo kikuu ni shinikizo la juu la damu au presha na ugonjwa wa kisukari.
“Shinikizo la juu la damu ambalo halijadhibitiwa, humweka mtu katika hatari kubwa ya kupata tatizo la figo, haimaanishi ukiwa na hayo magonjwa utapata shida hiyo, lakini usipodhibiti presha au sukari uwezekano wa kupata tatizo hilo ni mkubwa,” alisema Dk Kessy.
Pia, alisema unywaji holela wa dawa za kupunguza maumivu una madhara kwenye figo zikitumika kwa muda mrefu bila kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya.
Alitaja vyanzo vingine vya kufeli kwa figo kuwa ni mawe katika mfumo wa mkojo, uwepo wa mawe katika kibofu cha mkojo, maambukizi kama malaria kali na bakteria kwenye damu, inayosababisha maambukizi makali ya presha kushuka na kuwa chini.
“Uvimbe wowote usipotibiwa kwenye mfumo wa mkojo mirija ikiziba njia na ile njia isipofunguliwa ipo pia hatari ya kuleta madhara kwenye figo pamoja na maambukizi ya mara kwa mara ya mfumo wa mkojo (UTI) yanaweza kusababishwa figo kufeli,” alisema Dk Kessy.
Pia, alisema ili kuepuka kufeli kwa figo ni muhimu kuzingatia mtindo bora wa maisha, “ukiugua uende kuchunguzwa na kutibiwa, usienda kununua dawa pharmacy, ulaji tunashauriwa tule mlo kamili.”
Alisema kunywa maji mengi kutasaidia kuzuia kupata mawe kwenye figo, huku akisisitiza kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara kwa wataalamu na si maabara bubu.
Mzigo wa matibabu
Mkurugenzi wa Huduma za Wanachana wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Christopher Mapunda alisema matibabu ya figo kwa mwaka 2017/18 yalikuwa Sh16.54 bilioni, sawa na asilimia 62 huku mwaka 2018/19 yalikuwa Sh20.51 bilioni, sawa na asilimia 24.
“Mwaka 2019/20 mwenendo wa gharama za matibabu ya figo zilikuwa ni Sh27.16 bilioni, sawa na ukuaji asilimia 32 huku mwaka 2020/21 zikiwa Sh32.89 bilioni, sawa na ukuaji wa asilimia 21,” alisema.
Mapunda alisema mfuko huo umekuwa ukitumia wastani wa Sh35.8 bilioni kusafisha damu kupitia huduma ya dialysis.
Alisema awamu ya sita imewekeza kwenye huduma ya dialysis Sh1 bilioni kwa kununua mashine 77 zilizopo katika hospitali 11, gharama zikitarajiwa kupungua kutoka Sh300,000 mpaka Sh100,000.
Hata hivyo, Dk Linda alisema changamoto ni pamoja na rasilimali finyu za huduma ya magonjwa ya figo, ubora wa matibabu ya magonjwa ya figo, gharama kubwa za matibabu, kukosekana kwa mfumo wa udhibiti wa huduma ya magonjwa ya figo, kukosekana kwa mfumo wa taarifa za magonjwa ya figo.