Uhuru Afuta Kikao cha Ikulu Ghafla Kisa Hujuma





MKUTANO uliokuwa umeitishwa na Rais Uhuru Kenyatta leo katika Ikulu ya Nairobi kati yake na viongozi waliochaguliwa Mlima Kenya ulifutiliwa mbali dakika za mwisho jana, kwa hofu kwamba, wandani wa Naibu Rais William Ruto wangeuhujumu.

Duru zilieleza Taifa Leo kuwa, mkutano huo uliahirishwa baada ya kufahamika wanasiasa wa mrengo wa Dkt Ruto walipopata mwaliko huo walipanga ghafla mikutano katika maeneo bunge ya Gatundu Kusini na Kaskazini, Kaunti ya Kiambu, ambako Dkt Ruto angepokea wafuasi wa Jubilee wanaohama.

“Ingekuwa picha mbaya Dkt Ruto akiwa nyumbani kwa rais kupokea wahamaji huku rais akifanya kikao na wandani wake Ikulu,” Taifa Leo ilifahamishwa na duru za Ikulu.

Mkutano huo ulikuwa umeandaliwa kujadili mbinu za kuzima wimbi la Dkt Ruto katika Mlima Kenya, lakini ikaibuka haungekuwa na makali ikizingatiwa ungegeuzwa kuwa ajenda ya kudhalalishwa katika mikutano ya Dkt Ruto leo Kiambu.


Pia, ulikuwa mkutano wa kuidhinisha kutimuliwa kwa Kiranja wa Wengi katika Seneti, Kimani wa Matangi, ambaye Jumapili alijiunga na Dkt Ruto.

Naye Seneta wa Embu, Njeru Ndwiga, ambaye alihama Jubilee wiki hii alikuwa atimuliwe kutoka kamati ya Seneti kuhusu Kilimo.

Taifa Leo ilifahamishwa kuwa, mkutano huo ulikuwa pia uidhinishe kupokonywa marupurupu, maafisa wa usalama, nyumba na magari kwa maspika, viranja, viongozi wa wengi na wachache wa Jubilee katika mabunge ya kaunti ambao wamehama na kujiungia na chama cha Dkt Ruto. Kati ya waliolengwa ni Spika wa Kiambu Stephen Ndichu na mwenzake wa Nyeri John Kaguchia.


Spika wa bunge la Kitaifa Justin Muturi, ambaye amegura Jubilee na kujiunga na Democratic Party pia yumo kwenye orodha ya ambao wanapangiwa kuadhibiwa.

Ripoti kutoka Ikulu zilisema mkutano huo ulikuwa umepangwa pia kujadili jinsi ya kukabiliana na Dkt Ruto mlimani.

“Mkutano huo ulikuwa ni wa dharura na ulilenga kutafuta umoja wa chama cha Jubilee katika kukabiliana na wimbi la UDA, kuwa na msimamo

mmoja kuhusu ushirikiano na vyama vidogo pamoja na Jubilee ndani ya Azimio la Umoja, kuvumisha uwaniaji urais wa Raila na pia kupata uwiano kuhusu mchujo wa Jubilee,” akasema Mbunge wa Gatanga Nduati Ngugi.


Kuhusu ni kwa nini mwaliko huo ukatumwa hadi kwa wale ambao wamemuasi rais, Katibu Mkuu wa Jubilee, Jeremiah Kioni alisema rais amesema waziwazi kwamba katika safari ya kufanikisha Azimio

la Umoja atajadiliana na viongozi mbalimbali.

“Rais akiwa nembo ya umoja wa kitaifa ana jukumu la kupalilia umoja ndani ya Mlima Kenya. Tunataka kutembea safari hii kama Wakenya na rais hana kinyongo na wale ambao wamekuwa wakimkaidi. Lakini mkutano utaandaliwa siku nyingine hivi karibuni,” akasema Bw Kioni.

Hata hivyo, huku wale ambao wamekuwa wakiegemea mrengo wa rais wakisema wangefika Ikulu, wal – io na imani kwa Dkt Ruto walikuwa wamesema hawangehudhuria.


Mwaliko huo ulitumwa kupitia nambari maalum ya kiongozi wa wengi bungeni Amos Kimunya na ukafuatiliwa na kiranja wa wengi Maoka Maore akiwataka wafike bila kuchelewa.

Mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua alisema wafuasi wa Dkt Ruto wanaweza wakakutana na rais bora tu atumie “njia zifaazo” na pia aweke wazi ajenda ya mkutano huo.

“Hatuna shida kukutana na rais kama kiongozi wetu wa taifa, lakini kwanza atuhakikishie hatatushinikiza kumuunga mkono Raila. Pia ajenda ziwe kuhusu kupunguza bei ya fatalaiza kwa wakulima, gharama ya maisha kwa Wakenya na kukoma kuhangaisha wafuasi wa Ruto,”akasema.

Alisema huenda waandalizi walikuwa pia na nia ya kutaka kuwaonyesha wafuasi wa Dkt Ruto kuwa wakaidi iwapo wangekataa kuhudhuria.

Kauli hiyo ilithibitishwa na Mbunge wa Kangema, Muturi Kigano aliyesema: “Tulijua hawangeweza kuukubali mwaliko huo.” Mbunge wa Mwea Kavinga wa Thayu alisema mkutano huo licha ya kuahirishwa ulikuwa wa kuweka wazi ajenda ya Mlima Kenya ndani ya Azimio la Umoja.


“Ni katika mkutano huo ambapo tungejadiliana kuhusu masilahi yetu ndani ya serikali ya Azimio la Umoja, hakikisho kwamba tuliosimama na rais na Jubilee tutapata nafasi katika serikali hiyo, tuelewane kuhusu mbinu za mchujo na hatimaye jinsi ya kukabiliana na wapinzani wetu,” akasema Bw Kavinga.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad