Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanakuta huko Versailles kujadili gesi ya Urusi na uhusiano na Ukraine.
Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanakuta huko Versailles kujadili gesi ya Urusi na uhusiano na Ukraine. © REUTERS/Sarah Meyssonnier
Hospitali ya akina mama wajawazito kujifungulia na wodi ya watoto zimeshambuliwa na ndege ya kivita ya Urusi katika mji wa Mauripol nchini Ukraine na kusababisha vifo vya watu 17 na kuwajeruhi wengine.
Kitendo hicho cha Urusi kimelaaniwa na viongozi wa dunia huku, rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky akielezea kitendo hicho cha Urusi kama uhalifu wa kivita.
Baada ya shambulizi hili ambalo pia limelaaniwa na Umoja wa Mataifa, Zelensky ameendelea kutoa ombi kwa mataifa ya Magharibi ya kuweka marufuku ya ndege za kivita za Urusi kutopaa katika angalaa la Ukraine ili kuepusha mashambulizi mengine.
Wakati hayo yakijiri, uongozi wa mji wa Mauripol ulio Kusini mwa Ukraine, unasema watu zaidi yua 1200 wamepoteza maisha katika mji huo pekee tangu Urusi ilipoanza mashambulizi.
Nalo Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na watoto UNICEF, linasema watoto 37 wamepoteza maisha katika vita hivyo.
Wakati huu vita vikiendelea, watu Elfu 35 wamefanikiwa kukimbilia katika maeneo salama, kutoka katika miji mbalimbali ya Ukraine.