Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amepuuzilia mbali takwa la rais wa Urusi, Vladimir Putin la kuyataka mataifa ya Ulaya kununua gesi kwa sarafu ya Kirusi.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amepuuzilia mbali takwa la rais wa Urusi, Vladimir Putin la kuyataka mataifa ya Ulaya kununua gesi kwa sarafu ya Kirusi, huku akimshutumu rais huyo kuwa mwenye nia ya kutaka kuvikwepa vikwazo alivyowekewa kutokana na uvamizi wake wa Ukraine.
Macron aliwaambia waandishi wa habari baada ya Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Ulaya wa mjini Brussels kwamba hatua ya Urusi haipo katika makubaliano na haoni sababu ya kutekelezwa kwa jambo hilo. Rais Putin alitoa takwa hilo juma hili katikia kipindi hiki ambacho serikali yake inakabiliwa na vikwazo vikali vinavyoathiri uchumi wa taifa hilo, kutokana na hatua yake ya kuingia kijeshi nchini Ukraine.
Rais Joe Biden wa Marekani amesema Rais Vladimir Putin wa Urusi ameshindwa kuyagawanya mataifa ya Magharibi kwa vita vyake vya Ukraine. Umoja wa Kujihami wa NATO haujawahi kuwa pamoja kama ilivyo katika kipindi hiki. Rais Biden ambae alitua katika eneo la mpakani mwa Poland na Ukraine alisema Rais Putin amepata taswira tofauti kabisa baada ya uvamizi wake huo na kuongeza kwa kusema NATO itajibu mapigo kama Urusi itatumia silaha za kemikali.
Katika uwanja wa mapambano, jeshi la Urusi limesema idadi ya wanajeshi wake waliouwawa nchini Ukraine imefikia 1,351, waliojeruhiwa 3,825 na kuongeza kuwa limefanikiwa kuwaokoa raia 400,000. Akiyaeleza hayo mwakilishi wa mkuu wa majeshi wa Urusi, Sergei Rudskoi ameyahamakia mataifa ya Magharibi kwa kusema kupelekwa kwa silaha nchini Ukraine kunasababsisha kurefushwa kwa muda wa operesheni yao ya kijeshi.
Pamoja na kauli hiyo lakini silaha za nyongeza kutoka Ujerumani zimewasili nchini Ukraine. Silaha hizo ni pamoja na zana za kujikinga na makombora ya anga 1,500 aina nyingine ya MG, machine Gun 100. Kadhalika katika mzigo huo kuna aina milioni nane za silaha ndogondogo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Ujerumani DPA misaada mingine zaidi kutoka Ujerumani imeripotiwa kuingia katika ardhi ya taifa hilo ikiwemo madawa, makasha 350,000 ya chakula na magari ya kuwabebea wagonjwa.