Maelfu ya wakazi wa Jiji la Kyiv ambalo ndiyo Mji Mkuu wa Ukraine, wanaendelea kuukimbia mji huo ikiwa ni muda mfupi tangu Rais wa Urusi, Vladimir Putin atangaze vitisho vya kuwataka wakazi wa jiji hilo wakimbie au wabaki wafe wakati vikosi vya Jeshi la Urusi vyenye askari wapatao 15,000 vikianza mashambulizi ambayo Putin ameyaita kuwa ya kimkakati.
Jana usiku, Jumanne ya Machi Mosi, 2022 video zilikuwa zikisambaa kwa kasi mitandaoni, zikiwaonesha maelfu ya wakazi wa Jiji la Kyiv wakigombea kuingia kwenye treni ambazo tayari zilikuwa zimejaa, wakitafuta namna ya kuondoka kwenye mji huo.
Msafara mkubwa wa vikosi vya Jeshi la Urusi wenye urefu wa takribani kilometa 64, unazidi kusonga mbele kuingia katika Jiji la Kyiv huku mashambulizi makali yaliyolenga makazi ya watu yakisikika usiku kucha katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.
Miongoni mwa mashambulizi yaliyotingisha Jumanne usiku, ni shambulio la makombora lililoulenga mnara wa kurushia matangazo ya runinga jijini Kyiv wenye urefu wa futi 1,300 pamoja na makumbusho ya mauaji ya halaiki ya Babyn Yar Holocaust Memorial ambapo watu takribani watano wanaripotiwa kupoteza maisha.
Makumbusho ya mauaji ya halaiki ya Babyn Yar Holocaust Memorial, ndipo walipozikwa watu takribani 150,000 ambao waliuawa katika vita kati ya Adolf Hitler na Jamhuri ya Kisovieti ya Urusi (USSR) mwaka 1941, wakiwemo wayahudi 34,000.
Muda mfupi baada ya shambulio hilo, Rais Kushambuliwa kwa makumbusho hayo, Rais Volodymyr Zelenskyy kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Twitter, aliandika ujumbe kuonesha kusikitishwa kwake na hatua hiyo ya Urusi.
“Kwa dunia nzima, kuna maana gani ya kusema haitajirudia tena kwa miaka 80 ikiwa dunia ipo kimya wakati mabomu yakiangushwa katika eneo lilelile la Babyn Yar? Watu watano wamefariki dunia. Historia inajirudia,” ulisomeka ujumbe huo wa Rais Zelenskyy.
Kutokana na nguvu kubwa iliyoanza kutumika na Jeshi la Urusi, wachambuzi wa masuala ya vita wanakadiria kwamba hautapita muda mrefu kabla ya majeshi ya Urusi hayajauteka mji huo na kuipindua rasmi serikali ya Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine.
Hapo jana pia majeshi ya Urusi yaliupiga mji wa pili kwa ukubwa nchini Ukraine, Kharkiv na kusababisha vifo vya watu 11 huku wengine kadhaa wakijeruhiwa.
Hospitali nyingi zimeendelea kufurika majeruhi wa mashambulizi hayo huku mamlaka nchini Ukraine zikieleza kwamba majeshi ya Urusi yalikuwa pia yakiwashambulia wanawake na watoto waliopewa hifadhi katika maeneo salama.
Shambulio lingine limepiga jirani na hospitali katika Mji wa Zhytomyr uliopo Kaskazini mwa Kyiv ambapo meya wa mji huo, Serih Sukhomlin ameandika kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Facebook akieleza kwamba watu wawili wamefariki dunia katika shambulio hilo na nyumba kadhaa kuharibiwa, ikiwemo kuvunjika kwa madirisha ya hospitali