Wakati Rais wa Marekani, Joe Biden akiendelea na ziara yake ya siku mbili ya kuwatembelea wakimbizi wa Ukraine waliopo nchini Poland, majeshi ya Urusi yameushambulia Mji wa Lviv uliopo jirani na mpaka kati ya Ukraine na Poland na kusababisha uharibifu mkubwa huku watu watano wakifariki dunia.
Shambulio hilo limetekelezwa jioni ya Jumamosi katika Mji wa Lviv, umbali wa takribani kilometa 390 kutoka mahali alipo Rais Biden, katika kile kinachotajwa kwamba ni vitisho vya wazi vya Rais Vladimir Putin kwa Biden ambaye taifa lake limekuwa na uhasimu wa muda mrefu na Urusi.
Moshi mzito na moto vimeonekana katika anga la Lviv baada ya shambulio hilo la makombora matatu ambalo linatajwa kuwa ndiyo kubwa zaidi kuwahi kutokea katika Mji wa Lviv tangu majeshi ya Urusi yalipoanza uvamizi wake nchini Ukraine.
Picha kadhaa zimesambaa kwenye mitandao ya kijamii zikionesha nyumba za makazi ya watu zikiwa zimeharibiwa vibaya na shambulizi hilo la makombora.
Muda mfupi baadaye, wakati akihitimisha ziara yake nchini Poland, Rais Biden ametoa matamshi makali dhidi ya utawala wa Kremlin akieleza kwamba Rais wa Urusi, Vladimir Putin hawezi kusalia madarakani baada ya kuivamia Ukraine huku akiyaonya majeshi Urusi kutojaribu kusogeleea eneo la jumuiya ya kujihami ya NATO.
Rais Biden pia ameongeza kuwa vita vya Urusi dhidi ya Ukraine ni mkakati wa Moscow ulioshindwa, matamshi ambayo yameamsha upya vuguvugu kati ya Marekani na Urusi.
Kufuatia matamshi hayo, ikulu ya Washington imetolea ufafanuzi kuwa Rais Biden hakumaanisha kutoa wito wa Serikali ya Putin kuondolewa madarakani huku ikulu ya Kremlin nayo ikijibu kauli hiyo kwa kueleza kwamba Rais wa Urusi alichaguliwa na raia wa Urusi na hawezi kuondolewa madarakani kwa matakwa ya watu ambao siyo raia wa Urusi.