Urusi inadai imeudhibiti kabisa Mji wa Kherson nchini Ukraine, huu putakuwa ni Mji wa kwanza kudhibitiwa na Urusi tangu uvamizi wake ulipoanza nchini humo.
Wakati huohuo Wanajeshi wa Urusi wamewasili katika Mji wa Kharkiv, Mji wa pili kwa ukubwa wa Ukraine, Rais wa Ukraine Volodymir Zelensksy ameikosoa hatua ya Urusi kuishambulia Miji yenye idadi kubwa ya Watu akiitaja kuwa ni kampeni ya ugaidi.
Rais Zelensky amesema hakuna atakayesamehe wala kusahau umwagaji damu katika uwanja wa Kharkiv na shambulizi la bomu dhidi ya mnara wa televisheni katika mji mkuu Kiev, ambalo ameliita kuwa ni kitendo cha ugaidi na uhalifu wa kivita.
Mashambulizi katika Mji wa Kharkiv yameendelea leo huku Urusi ikikishambulia kituo cha polisi na makao makuu ya idara ya ujasusi, Idara ya kitaifa ya huduma za dharura ya Ukraine imeripoti kuwa watu watatu wamejeruhiwa katika hujuma hiyo, wakati hayo yakijiri Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez ameliambia Bunge leo kwamba Nchi yake itatuma silaha Ukraine.