Urusi yaongeza mashambulizi katika miji ya Ukraine



Mji wa bandari wa Mariupol umezingirwa na kushambuliwa kwa makombora, na mji mkuu wa Ukraine Kyiv pia wakabiliwa na mashambulio mapya. Uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine unaendelea kwa wiki ya pili sasa.

Russland-Ukraine Krieg Angriff Irpin
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litaitisha mkutano wa dharura kujadili mgogoro wa kibinadamu uliosababishwa na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.  Shirika la habari la AFP lememnukuu mwanadiplomasia mmoja aliyesema baada ya kikao cha Baraza la Usalama kilichopangwa kufanyika siku ya Jumatatu, wajumbe 15 wa baraza hilo watakutana kwa faragha kutafakari juu ya uwezekano wa kupitishwa rasimu ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Mkutano huo wa faragha umependekezwa na Mexico na Ufaransa.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Nchi hizo mbili zimekuwa zikishinikiza kuwepo kwa rasimu inayotaka kusitishwa kwa mapigano nchini Ukraine na kutaka kufikishwa kwa misaada ya kibinadamu na ulinzi wa raia nchini humo. Urusi, kama mwanachama wa kudumu mwenye kura ya turufu kuna uwezekano mkubwa kuwa itapinga kupitishwa azimio lolote na Baraza la Usalama, dhidi yake.

Wakati huo huo Katibu mkuu wa jumuiya ya kijeshi ya NATO Jens Stoltenberg ametahadharisha juu ya kutokea vifo zaidi, maafa na madhara makubwa kutokana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Wakati huo huo mfungamano wa kujihami wa NATO na Marekani zimekataa wito wa Ukraine wa kuilinda anga ya nchi hiyo kwa kuhofia kuingia vitani na Urusi. Mawaziri wa nchi za NATO walitoa kauli hiyo baada ya mkutano wao wa mjini Brussels siku ya Ijumaa.


 
Katibu mkuu wa Jumuiya ya kijeshi ya NATO, Jens Stoltenberg
Katibu mkuu wa Jumuiya ya kijeshi ya NATO, Jens Stoltenberg

Katibu mkuu wa jumuiya hiyo ya kijeshi Jens Stoltenberg ameeleza kuwa NATO haimo katika mgogoro baina ya Urusi na Ukraine lakini washirika wa NATO wana wajibu wa kuzuia kuenea kwa vita vya nchini Ukraine.  Amesema endapo vitaenea hatari itakuwa kubwa zaidi na italeta maafa kwa binadamu. Hata hivyo mawaziri wa nchi za NATO waliokutana mjini Brussels wameahidi kuweka vikwazo zaidi dhidi ya rais wa Urusi Vladimir Putin.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken aliyehudhuria mkutano wa mjini Brussels amesema mfungamano wa kijeshi wa NATO utalinda kila sehemu ya nchi wanachama na kwamba Urusi isipuuze azma hiyo ya Marekani. Ameeleza kuwa mfungamano wa NATO ni wa kujihami na kwamba NATO haitaki mzozo lakini ikiwa itapelekewa mzozo itakuwa tayari.


Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani amesema NATO itaendelea kuibana Urusi mpaka pale itakapobadilisha mwenendo wake.Nato itaendelea kuitenga Urusi na kuiumiza kiuchumi. Msaada uliotolewa kwa ajili ya Ukraine mpaka sasa ni silaha kutoka nchi za NATO na za magharibi kwa jumla, sambamba na vikwazo vilivyowekwa vya kiuchumi vilivyowekwa dhidi ya Urusi.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amelaumu hatua hiyo ya NATO na kusema kuwa ni sawa na kuidhinisha mashambulizi zaidi ya Urusi dhidi ya nchi yake. Zelenskyy ametoa wito kwa jumuiya ya NATO kuilinda anga ya nchi yake. Ukraine pia inataka kujiunga na NATO na pia kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya. Urusi inapinga lengo hilo la Ukraine na imesema kuwa usalama wake utatishiwa. Majeshi ya Urusi yamezishambulia kwa mizinga sehemu za raia na imeteka, mitambo miwili ya nyuklia nchini Ukraine.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad