Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Vassily Nebenzia, amesema nchi yake itasitisha mapigano kuanzia saa nne asubuhi ya leo kwa majira ya Moscow na kufunguwa njia salama kuwahamisha raia kutoka miji ya Kiev, Cher-nigov, Sumy na Mariupol.
Kwa mujibu wa Nebenzia, pendekezo hilo halina masharti yoyote kwa raia wanaopitia Urusi. Rais Volodymyr Zelenskiy amesema badala ya kutangaza makubaliano ya kuwepo kwa njia salama, Urusi inaongeza vifaru, makombora na mabomu.
Wote wawili wamezungumza baada ya duru ya tatu ya mazungumzo kati ya Ukraine na Urusi iliyomalizika jioni ya jana. Pande zote mbili zimetangaza kupigwa kwa hatua kwenye mazungumzo hayo.
Hata hivyo, Rais Zelensky amelikataa pendekezo la kuwapitishia raia wa nchi yake kwenye kile alichokiita “ardhi ya mvamizi.” Akizungumza akiwa ofisini mwake mjini Kiev, Zelensky ameapa kuendelea kusalia ndani ya nchi kuongoza mapambano.