MSEMAJI wa Ikulu ya Kremlin ya Urusi, Dmitry Peskov amesema Urusi itatumia silaha za nyuklia endapo uwepo wa taifa hilo utakumbwa na vitisho.
Peskov ameyasema hayo hapo jana wakati akihojiwa na mwandishi wa habari wa Shirika la Utangazaji la CNN, Christiane Amanpour aliyembana kwa maswali akitaka atoe maoni yake kama Rais Vladimir Putin anaweza kutumia silaha za nyuklia nchini Ukraine.
“Tunao mpango wa masuala ya ulinzi wa ndani, na kila mmoja anaujua. Unaweza kusoma na kuona sababu zinazoweza kutufanya tutumie silaha za nyuklia.
“Kwa hiyo kama ni suala linalotishia uwepo wa taifa letu, basi silaha za nyuklia zitatumika kwa mujibu wa mpango,” alikaririwa Peskov katika mahojiano hayo yaliyofanyika Jumanne ya Machi 22, 2022.
Peskov ameiambia CNN kwamba uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, unaenda kama mipango ilivyopangwaawali.
Maelezo hayo ya Peskov yamekuja katika kipindi ambacho Rais wa Marekani, Joe Biden ameonya kwamba Rais Putin anafikiria kutumia silaha hatari za maangamizi ya halaiki nchini Ukraine na kuongeza kwamba majeshi yake yanafanya ukatili mkubwa kwa raia.
Kauli hiyo ya msemaji huyo wa ikulu, pia inakuja mwezi mmoja tangu Rais Putin alipovitaka vikosi vyake vya nyuklia kukaa katika hali ya utayari, jambo lililozua hofu duniani kote kuhusu mpango wa Urusi kutumia silaha za nyuklia.
Mbali na agizo hilo, Waziri wa Ulinzi wa Urusi, Sergei Shoigu, Februari 28, 2022 alinukuliwa na Shirika la Habari la Interfax akieleza kuwa silaha za nyuklia za Urusi katika vikosi vilivyopo Kaskazini mwa nchi hiyo na katika Bahari ya pacific, vipo kwenye hali ya utayari kusubiri maelekezo yoyote kutoka kwa mamlaka za juu.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres. Machi 14, 2022 alinukuliwa akisema mgogoro wa nyuklia ambao awali ulikuwa unaonekana kama ni kitu kisichoweza kufikiriwa, sasa umerejea kwa kasi na inaonesha ni kitu kinachowezekana.
Wiki iliyopita, Urusi ilikiri kutumia makombora ya Hypersonic ambayo ni miongoni mwa silaha zilizopigwa marufuku na Umoja wa Mataifa kutumika vitani, yakiwa na uwezo wa kusafiri kwa umbali mrefu ndani ya muda mfupi na kusababisha madhara makubwa