Ndoa ya Mwenyekiti wa Chama cha TLP, Augustino Mrema imeibua utata na kusemekana kuwa ni batili kufuatia uwepo wa madai kuwa mwanamke aliyefunga nae ndoa, Doreen Kimbi, ni mke wa mtu.
Na inasemekana kwamba katika hafla fupi iliyofanyika baada ya ndoa hiyo iliyofungwa katika Kijiji cha Kiraracha, Marangu, haikuhudhuriwa na ndugu wa damu wa Doreen, isipokuwa marafiki zake wachache.
Kwa mujibu wa gazeti la Raia Mwema lililoripoti taarifa hiyo ni kwamba, ndugu wa karibu wa mwanamke huyo amesema hawakupewa taarifa juu ya ndoa hiyo na wameshangazwa kuona picha za ndugu yao akila kiapo cha pili cha ndoa.
Taarifa zinadai kuwa Doreen alifunga ndoa na Fredrick Mushi katika Kanisa Katoliki la Kristu Mfalme, Tabata mkoani Dar es Salaam na kujaaliwa mtoto mmoja, na baadaye kushindwa kuendelea na maisha ya ndoa baada ya kudaiwa kuwa mumewe aliondolewa kazini na kushindwa kuihudumia vyema familia yake.
“Mwaka 2019 mwanamke baada ya kuona kuwa ndiye anayemlea mume, akamkimbia na kwenda kuishi Moshi ambako alifungua biashara ya maua na upishi, hizo biashara zingine alizosema kwa kweli hatuzifahamu,” alisema ndugu huyo.
Kwa mujibu wa ndugu wa Doreen, wanasema wameshangazwa juu ya kauli ya Mrema kuwa alifika nyumbani na kukubaliana kuhusu mahari bila wazazi, kaka na dada zake kujua chochote.