VAR: Bado tafsiri ya kuotea ina ukakasi kwa waamuzi wa mpira wa miguu



Dar es Salaam. Wawakilishi wa Tanzania katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Simba wameweka matumaini ya kufuzu hatua ya mtoano baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya RS Berkane ya Morocco.

Mchezo huo ulikuwa na msisimko na ushindani wa hali ya juu na kusababisha kuwepo kwa matukio kadhaa ya kutatanisha kutoka kwa waamuzi waliotoka DR Congo.

Tukio la kwanza ni kuhusiana na bao alilofunga Pape Ousmane Sakho katika dakika za mwisho za kipindi cha kwanza kuwa halikuwa halali kutokana na sheria za mpira wa miguu.

Hatua hiyo imefikia kuwagawa mashabiki wa soka katika mitandao mbalimbali ya kijamii kuhusiana na uhalali wa bao hilo.


 
Asilimia kubwa ya mashabiki wa Simba

wanasema hilo ni bao halali na kumuunga mkono mwamuzi wa mechi hiyo kwa uamuzi mzuri alioufanya. Pia kuna ukinzani kutoka kwa mashabiki wa mpira wengi wakisema mwamuzi ameibeba Simba kwa kukubali bao ambalo si halali.

Hoja nyingi zimetolewa kuhusiana na matakwa ya sheria namba 11 ambayo ni kuzidi (kuotea au offside) kwa mujibu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (Fifa). Sheria hiyo ina vipengele vingi, lakini kwa mechi ya Simba dhidi ya RS Berkane kipengele kinachotajwa ni kitendo cha kuingilia mchezo.

Tukio la pili linahusha kipa wa Simba, Aishi Manula aliyedaiwa kumfanyia faulo mchezaji mmoja wa RS Berkane katika dakika ya 63 ya mchezo ambapo mwamuzi kutoka DR Congo, Jean Jacques Ndala hakutoa uamuzi wa pigo la penati.


Pia kulikuwa na tukio katika dakika 82 ya mchezo ambapo mwamuzi msaidizi namba moja alikataa bao lililofungwa na Hamza Regragui ambaye alisema alikuwa amezidi (ameotea).

SHERIA INASEMA

Katika tukio la kwanza ambao lilizaa bao pekee katika mchezo huo kabla ya Sakho kufunga, kulikuwa na wachezaji wawili wa Simba, Meddie Kagere na Rally Bwalya ambao walikuwa katika nafasi ya kuotea.

Bwalya alikuwa pembeni ya kipa wa RS Berkane na hakuonekana kuingilia mchezo. Kitendo hicho kilimfanya kipa wa RS Berkane kutokuwa na umakini naye na kuelekeza umakini wake kwa eneo la mpira mbele ya Kagere na amchezaji aliyefunga, Sakho.

Kwa mujibu wa sheria namba 11 ambayo ni kuzidi (kuotea au offside) kwa mujibu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA), Bwalya hakuingilia mchezo.


 
Kagere anahukumiwa kuwa alikuwa amezidi kwa sababu kubwa zifuatazo. Kwanza, kumzuia kipa kuona moja kwa moja kutoka kwa mpigaji mpira (preventing an opponent from playing or being able to play the ball by clearly obstructing the opponent’s line of vision) na sababu ya pili ni kuingilia mchezo (kwa kuruka juu) na kumfanya kipa wa Berkane kushindwa kuona moja kwa mpira uliopigwa na Sakho (making an obvious action which clearly impacts on the ability of an opponent to play the ball).

Hata hivyo, inawezakana kabisa mwamuzi alitumia kigezo cha umbali ambao Kagere alikuwepo kati yake na kipa wa Berkane.

Ni wazi kuwa kulikuwa na uwezo wa kipa huyo kuona mpira na ndiyo maana mwamuzi aliruhusu goli la Simba.

Hivyo tunaweza kusema kuwa halikuwa goli halali kwa kigezo cha sheria za Fifa na vilevile ni goli halali kwa maono ya mwamuzi hasa kwa kuzingatia umbali kati ya mpigaji mpira (Sakho), Kagere na kipa.


Tukio la pili

Mwamuzi Jean Jacques Ndala alilalamikiwa na viongozi wa RS Berkane kwa kuwanyima penalti katika dakika ya 63 ya mchezo na kuzua mtafaruku. Tukio hilo lilimhusisha kipa wa Simba, Aishi Manula ambaye alikwenda kuzuia mpira akiwa eneo na hatari na mchezaji wa Berkane kuanguka.

Ukiangalia picha za marejeo, ni wazi kuwa Manula ndiye alikuwa wa kwanza kufikia mpira na kuucheza kabla ya mchezaji wa Berkane ambaye alijirusha na kuangukia nyuma ya Manula.

Hivyo haikuwa penalti kama ilivyodaiwa na wachezaji na viongozi wa RS Berkane.

Tukio la tatu

Zikiwa zimesalia dakika nane mpira kufikia tamati, RS Berkane walifunga bao ambalo lilikataliwa na mwamuzi msaidizi wa kwanza. Ukiangalia picha za marejeo, bao hilo lilikuwa halali kwani mfungaji hakuwa eneo la kuzidi pamja na baadhi ya wachezaji wa timu ya RS Berkane walikuwa wamezidi.

Mwamuzi msaidizi namba moja alizingatia zaidi wachezaji ambao walikuwa kwenye mstari wa kuotea, lakini hawakuingilia mchezo na walikuwa mbali zaidi.


 
Ila uamuzi wa mwamuzi ndiyo wa mwisho akiwa uwanjani.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad