Rais wa Senegal, Macky Sall, ambaye ni mkuu wa sasa wa Umoja wa Afrika (AU), amezungumza na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin kuhimiza usitishaji vita "wa kudumu" nchini Ukraine.
Yeye ni kiongozi wa pili wa Afrika kufichua kwamba amewasiliana na Bw Putin - mwingine ni Rais wa Misri Abdul Fattah al-Sisi.
Katika ujumbe wake wa Twitter, Bw Sall alisema: "Kama rais wa Umoja wa Afrika, nimefurahishwa na mazungumzo yangu asubuhi ya leo na Rais Putin kushinikiza kusitishwa kwa mapigano kwa kudumu.
"Ninampongeza kwa kusikiliza na kwa nia yake ya kudumisha mazungumzo kwa ajili ya matokeo ya mazungumzo ya mzozo."
Ofisi ya Bw Sisi ilisema mazungumzo yake na Bw Putin yalilenga mzozo wa Ukraine, na kuimarisha uhusiano kati ya mataifa hayo mawili.
Baada ya wanajeshi wa Urusi kuingia Ukraine tarehe 24 Februari, AU ilitoa taarifa ikitaka Ukraine kuheshimiwa na sheria ya kimataifa kuzingatiwa.
Jumuiya ya kanda ya Afrika Magharibi Ecowas ilisema inalaani uvamizi huo.