Jeshi la Polisi nchini Afrika Kusini (SAPS) limeanza msako huko Mpumalanga dhidi ya washukiwa watatu waliovamia kanisa moja lililopo Thulamahashe karibu na Bushbuckridge na kuwabaka wanawake wawili kisha kuondoka na gari la mchungaji na vyombo vya muziki.
Tukio hilo limetokea Machi 18 na wanawake walioathirika wana umri wa miaka 30 na 38 kwa mujibu wa taarifa ya msemaji wa SAPS Brigadier Selvy Mohlala.
Kuhusu kilichotokea, polisi wa Mpumalanga wanasema wanawake wawili walikuwa kwenye chumba kimoja ndani ya kanisa hilo mwendo wa saa 5:00 usiku, walisikia mlio wa risasi kisha mlango ukagongwa.
Watu watatu wakiwa na silaha waliingia ndani kwa nguvu.
“Waliwashikilia wanawake hao wakiwa wamewaelekezea bunduki huku wakijaribu kujua mahali alipokuwa Mchungaji. Washukiwa hao walitaka pesa taslimu na inadaiwa waliwabaka wanawake hao,” amesema Mohlala.
Washukiwa hao pia walichukua vyombo vya muziki vya kanisa hilo vyenye thamani ya takribani Sh milioni 4.3 (R28,000), wakitumia gari aina ya KIA Picato ya rangi ya silver, mali ya Mchungaji wa kanisa hilo.
Polisi wamewataka wananchi ambao wanaweza kuwa na taarifa zinazohusiana na kesi hiyo kujitokeza.