Wafanyabiashara Dodoma wagomea soko la Job Ndugai



Dodoma. Wafanyabiashara wa ndizi na viazi katika soko la Majengo wanadai kuumizwa na agizo la Mkurugenzi wa Jiji, Joseph Mafuru la kuwataka kushushia bidhaa zao kwenye soko la Job Ndugai.

Hivi karibuni Mkurugenzi Jiji aliwataka wafanyabiashara kutokushusha bidhaa za vyakula kama ndizi, viazi, matunda na mbogamboga kwenye Soko la Majengo.

Mwananchi lilifanya mazungumzo na wafanyabiashara hao ambao walidai kupata hasara ya usafirishaji na kupoteza ubora wa bidhaa kutokana na kugeuzwa geuzwa mara kadhaa.

Muzamilu Mohammed, mfanyabiashara wa viazi alisema kusafirisha bidhaa hizo huwapa hasara, kwani hupoteza fedha nyingi kufikisha kwenye masoko ya mjini.


 
Alisema bei ya kusafirisha viazi kutoka Mbeya hadi Dodoma, kisha kushusha soko la Majengo huwa tofauti ukilinganisha na kushusha bidhaa hiyo kwenye soko la Job Ndugai.

Soko la Majengo

Muzamilu alisema kusafirisha gunia la viazi kutoka Mbeya kwa lori aina ya scania mende ambalo linabeba gunia 200 ni Sh2,200,000 na kila gunia hugharimu Sh11,000.

Alisema magunia hayo yanashushwa na kusambazwa katika maghala yao sokoni hapo kwa Sh1,500 kwa kila gunia au kikundi cha watu kwa gharama isiyozidi Sh100,000, hivyo kufanya jumla ya gharama isiyozidi Sh400,000 ya ushushaji na usambazaji.


Alisema baada ya kushusha wanalipia Sh40,000 ya usafi kwa kila lori litakaloingia kushusha bidhaa hizo na wauzaji wa reja reja hufuata mzigo kwao.

“Ukiangalia hapo sisi huchangia kiasi kisichozidi Sh300,000 au 400,000 lakini kwa upande wa Ndugai hali ni mbaya kabisa,” alisema.

Kushusha bidhaa

Joseph Isaya, mfanyabiashara wa ndizi na viazi alisema baada ya kupakia lori kwa Sh 2,200,000 mkoani na kufika sokoni hapo, linatakiwa kushushwa na kikundi cha watu kwa Sh200,000 kwa kila lori.

Alisema baada ya kushushwa, wanalipa Sh40,000 ya usafi kwa lori na kuwafanya kuacha Sh240,000 kwenye soko huku kazi ya kupakia magunia hayo tena kwa ajili ya kufikisha kwenye masoko ya mjini ikiwasubiri. Kwa mujibu wa Joseph, baada ya hapo huchukua gari “kirikuu” ambayo ina uwezo wa kupakia gunia 10 na alieleza ili kupunguza gharama hulazimika kupakia hadi gunia 15.


 
“Kwa mtu ambaye ana gunia 200 ukizileta mjini kwa kila trip (safari) gunia 10 ambayo huwa Sh30,000 ni sawa na Sh600,000 ambayo tunaitumia kwa ajili ya usafirishaji. Yaani ukijumlisha ushushaji, usafi Sh400,000 na usafirishaji tunajikuta tunaacha Sh840,000 ambayo ni hasara kwetu kwa kweli,” alisema.

Alieleza kwa upande wa ndizi, kusafirisha mkungu mmoja kutoka shambani mkoani Njombe ni kuanzia Sh8,000 hadi Sh10,000 kwa mkungu.

Alisema gari aina ya scania Mende wastani hubeba mikungu 300 hadi 400 na kufanya bei ya kawaida ya usafirishaji kuwa zaidi ya Sh2,700,000.

Alisema kwa kawaida mkungu mmoja huwa na ndizi 100 ambazo wao wakiuza kwa kawaida hupata faida ya wastani wa Sh3,000 hadi 4,000. “Kutokana na shusha, pakia ya huko kote bidhaa kama ndizi haichelewi kubadilika rangi na kuoza, sasa ukiileta hapa mteja hanunui kwa jinsi ilivyo na baada ya muda mfupi tunatupa. Kule hakuna wateja, kwa hiyo kinachofanyika sasa tunatoa viazi na ndizi mikoani tunapeleka Ndugai halafu tena inatulazimu kukodi magari kuleta mjini,” alisema.


Ombi kwa mkurugenzi

Wafanyabiashara hao wamemuomba Mkurugenzi wa Jiji kusikiliza matakwa yao kutokana na hali hiyo wanayodai kuwaumiza.

Hata hivyo, walidai kusitisha kuleta bidhaa hizo mpaka zuio hilo litakapoondolewa kwa madai ya kukosa faida na fedha ya marejesho ya mikopo waliyokopa benki.

“Sio kama tumegoma, kilichopo tumeacha kuagiza biashara hii kutokana na hasara tunazozipata. Hatuwezi kuweka mitaji yetu ambayo inateketea kwa ajili ya kuwanufaisha walaji,” alisema Muzamilu.

Bishara rejareja

Kutokana na hali ya baadhi ya wafanyabiashara hao kusitisha na kushusha bidhaa hizo kwenye soko la Job Ndugai, kumechangia kupanda kwa bei ya bidhaa hizo kwa mfumo wa rejareja.

Issa Yusuph, muuza chipsi eneo la Majengo alisema bei ya viazi imepanda, hali inayowalazimu nao kupandisha bidhaa hiyo.


 
“Viazi hakuna kabisa na ukipata basi kwa bei ya juu, kwa hiyo na sisi lazima tupandishe bei ili tupate faida. Anayeumia sasa ni mlaji,” alisisitiza.

Issa alisema kwa sasa chips mayai anauza Sh3,000 huku chips kavu akiuza kati ya Sh2,000 hadi 2,500 kulingana na bei ya gunia la viazi watakalonunua kwa siku hiyo.

“Kutokana na hali ya mvua viazi vimekomaa chini na vingekuwa vinauzika kwa bei ya kawaida ya Sh45,000 kwa gunia, lakini sasa hakuna viazi na vimepanda gunia ni Sh90,000 hadi 120,000, kwa sababu watu hawaendi kuchukua viazi,” alisema.

Muuza ndizi katika eneo hilo, Justin Kivale alisema kwa sasa wananunua mkungu wa ndizi Bukoba kwa Sh30,000 hadi 35,000 wakati awali uliuzwa kati ya Sh18,000 hadi 25,000.

Alisema mkungu wa ndizi mzuzu awali uliuzwa Sh15,000, lakini sasa unauzwa kati ya Sh25,000 hadi 28,000. Kutokana na ongezeko hilo, Kivale alisema anauza ndizi sita ndogo kwa Sh2,000 na ndizi tatu kubwa kwa Sh2,000 ili kurudisha faida kwa mkungu wanaonunua Sh35,000.

“Sasa hivi hali ndio hiyo, lakini kwa kawaida ndizi saba huuzwa Sh1,000, yaani mtu anapata rundo, lakini sasa mtu akija na Sh1,000 tunamfanyia ndizi mbili na kipande, vinginevyo hatuuzi kwa bei hiyo,” alieleza.

“Hii ni ile mikungu ambayo mtu ana shamba lake la migomba kumi ndio wanaoleta ndizi hapa, lakini za kutoka mikoani bado hatuzioni na kama unavyoziona hazina nuru ile ya ndizi nzuri kama ya mkoani na wakati mwingine zinakuja hata hazijakomaa, lakini tunachukua ili tusipoteze wateja,” alisema.

Ni uchafu uliokithiri

Mkurugenzi Mafuru alikiri kutoa katazo hilo na kusema kuwa ni kwa ajili ya uchafu uliokithiri kwenye soko ambalo linaonekana kuelemewa na mizigo hiyo.

Alisema mwanzoni wafanyabiashara hao walionyesha kukaidi, lakini sasa wameanza kuzoea, lengo likiwa kunusuru afya za walaji.

“Hakuna cha hasara, mabadiliko yoyote lazima yaanze kwa mvutano, soko la Majengo ni langu na Job Ndugai ni langu na mimi ndo napanga hiki kikae hapa na hiki kikae hapa kwa ajili ya mipango miji,” alisema

Aidha, alisema kutokana na mazingira yaliyopo eneo hilo ni lazima hatua zichukuliwe, hususan katika kipindi cha mvua.

“Iko hivyo na haibadiliki, hata ukienda kuangalia sasa huwezi kununua matunda kwa sababu hali ni mbaya, kwa hiyo turuhusu waendelee ili watu wapate kipindupindu!?

“Lakini ukienda Job Ndugai soko ni zuri na la kisasa, wanashusha sehemu safi na salama, sasa ili twende sawa lazima mabadiliko yafanyike,” alisisitiza.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad