Washtakiwa 40 kati ya 85 wa kesi namba 12/2022 wakiwasili katika mahakama ta Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza kwa ajili ya kupewa dhamana. Picha Mgongo Kaitira.
Mwanza. Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Mwanza imewaachia kwa dhamana washtakiwa 40 kati ya 84 wa kesi namba 12/2022 inayomkabili Diana Bundala maarufu kama 'Mfalme Zumaridi' na wafuasi wake.
Mfalme Zumaridi na wafuasi wake walifikishwa katika mahakama hiyo Machi 3,2022 na kusomewa mashtaka matatu ambayo ni kuzuia maofisa wa Serikali kutekeleza majukumu yao, kufanya mkusanyiko usiyo na kibali na shtaka la usafirishaji haramu wa binadamu lililokuwa likimkabili Mfalme Zumaridi peke yake ambalo ni jinai isiyo na dhamana.
Washtakiwa hao baada ya kusomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu mfawidhi mwandamizi wa Mahakama ya Mkoa wa Mwanza, Monica Ndyekubora kisha kupewa nafasi ya kupewa dhamana walikataa kupewa dhamana kwa madai kwamba wako tayari kuendelea kusota rumande na kiongozi wao.
Akizungumza baada ya kutolewa kwa dhamana hiyo wakili wa washtakiwa hao, Erick Mutta amesema dhamana hiyo imetolewa baada ya mshtakiwa namba moja wa shauri hilo (Mfalme Zumaridi) kuiomba mahakama hiyo kuwaachia kwa dhamana washtakiwa wanaoweza kudhaminika katika kesi hiyo.
Amesema baada ya ombi hilo kuwasilishwa ni washtakiwa 40 ndiyo wamekubali kudhaminiwa huku 45 wakikataa dhamana hiyo badala yake wameomba waendelee kusota rumande na kiongozi wao.
"Jitihada zilizofanyika kupitia mshtakiwa namba moja (Mfalme Zumaridi) za kuweza kuwashawishi wakubali dhamana ndiyo zimezaa matunda mpaka hawa 40 wakakubali kudhaminiwa, wengine wamekaa dhamana hiyo," amesema Mutta