Kamanda Polisi wa Kanda ya Dar es Salaam, Jumanne Murilo
JESHI la Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, linamshikilia Mkurugenzi wa Mtandao wa U-Turn, Allen Samwel Mhina na wenzake 13, kwa tuhuma za kusambaza video ya mgonjwa akiwa Wodi ya Uangalizi Maalumu (ICU), kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Taarifa hiyo imetolewa leo Alhamisi, tarehe 17 Machi 2022 na Kamanda wa Jeshi la Polisi katika kanda hiyo, ACP Jumanne Muliro, akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam.
Kamanda Muliro amesema, watuhumiwa hao wamekamatwa na Jeshi la Polisi, kwa kushirkiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ambapo wnaatuhumiwa kwa kosa la matumizi mabaya ya mtandao kinyume na sheria
“Jeshi linamshikilia Mhina (31), mkazi wa Temeke Mwembeyanga na wenzake 13 kwa tuhuma za kusambaza video katika mitandao ya kijamii kinyume na sheria, ikimuonyesha mmoja wa wagonjwa aliyekuwa amelazwa wodi ya ICU, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili . Suala lililoleta taharuki kwa hospitali hiyo na wafanyakazi wake,” amesema Kamanda Muliro.
Aidha, Kamanda Muliro amesema Polisi wanashikiria vfaa mbalimbali vya kielektroniki, ikiwemo kamera, kalamu, saa funguo, miwani, Laptop na memory card, ambavyo vinachunguzwa.
“Kitendo kinachotuhumiwa kufanywa na watuhumiwa hao kililenga kudhalilisha, kutia hofu au kuleta taharuki suala ambalo linalazimisha mamkala hizi mbili za kisheria kuchunguza kwa kina suala hilo. Uchunguzi ukikamilika watafikishwa kwenye vyombo vingine vya kisheria,” amesema Kamanda Muliro.
Licha ya kutotaja jina la mgonjwa huo, video inayodaiwa kusambazwa na Mhina na wenzake, ni ile inayomuonesha aliyekuwa Mbunge wa Mikumi, mkoani Morogoro, kupitia Chama cha Chadema, Joseph Haule ‘Prof. Jay’, akiwa ICU akipigania uhai wake.
Kufuatia kuvuja kwa video hiyo kuibua mjadala na sintiofahamu mtandaoni, uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, uliiomba TCRA ifanye uchunguzi ili aliyerekodi na kuisambaza akamatwe kwa ajili ya kuchukuliwa hatua.