Xi Jinping asema vita vya Ukraine vinatia wasiwasi





Kiongozi wa China Xi Jinping ameita vita vinavyoendelea Ukraine kuwa vya kutia wasiwasi. Xi ameyasema hayo leo baada ya mazungumzo ya video na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, ikiwa ni siku ya 12 ya uvamizi wa Urusi kijeshi dhidi ya jirani yake. 

Serikali ya China haijalaani wala kuunga mkono mashambulizi hayo yanayofanywa na mshirika wake na imejizuia kuiita hatua hiyo "uvamizi". Nchi za Magharibi zimekuwa zikiitazama Beijing kuona kama ingeweza kuchukua jukumu la upatanishi katika mzozo huo. 

Ijapokuwa amesisitiza kuwa uhuru na mamlaka ya mipaka ya nchi zote lazima viheshimiwe, Xi pia amesema maslahi ya kiusalama ya nchi zote lazima yachukuliwe kwa umuhimu. Kiongozi huyo wa China amezipongeza juhudi za upatanishi zinazofanywa na Ujerumani na Ufaransa. 

Xi pia amezungumzia vikwazo vilivyowekewa Urusi akisema vinaathiri sekta za kifedha, nishati, usafiri na pia uimara wa uzalishaji na uuzaji bidhaa duniani, na hivyo kurudisha nyuma uchumi wa kimataifa unaoyumba kutokana na janga la corona.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad