HESABU za Yanga ni kupata ushindi katika michezo mitano ijayo ikiwemo dhidi ya Azam na Simba ili ijiwekee mazingira rahisi ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.
Lakini wakati Yanga wakiwa na hesabu hiyo, kocha wao Nasreddine Nabi yeye akipata ushindi au kutopoteza mechi moja tu inayofuata za Yanga atazidi kuimarisha rekodi ambayo inaweza kuwa mfupa mgumu kwa makocha wengine kuivunja.
Rekodi hiyo ni ile ya kuwa kocha aliyepoteza mechi chache zaidi za Ligi Kuu Tanzania Bara tangu alipowasili nchini na pia kuruhusu idadi ndogo zaidi ya mabao kulinganisha na wengine hapo nyuma.
Nabi ambaye Aprili 20 atatimiza muda wa mwaka mmoja tangu alipoanza kuitumikia Yanga, chini yake timu hiyo imepoteza mchezo mmoja tu wa ligi ambapo ilikuwa ni msimu uliopita walipofungwa bao 1-0 na Azam FC, ambao ulikuwa wa kwanza kwake tangu alipoanza kuinoa timu hiyo.
Baada ya hapo Nabi hajapoteza mchezo mwingine wowote wa Ligi Kuu ambapo ameiongoza Yanga katika jumla ya mechi 26 katika Ligi Kuu ambapo kati ya hizo timu hiyo imeibuka na ushindi mara 20 na imetoka sare mara tano.
Wakati Yanga ikipoteza mechi moja tu chini ya Nabi kwa mwaka mmoja alioifundisha, Simba imepoteza mechi tatu za Ligi Kuu ikiwa na makocha wawili tofauti huku ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara 10 wakati Azam imepoteza mechi sita na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 19.
Msimu uliopita aliiongoza Yanga katika mechi nane akipata ushindi mara tano, kutoka sare mbili na kupoteza moja, timu hiyo ikifunga mabao 11 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara tano wakati msimu huu ameshaiongoza timu hiyo katika michezo 18, ikiibuka na ushindi mara 15 na kutoka sare kwenye mechi tatu, ikifunga mabao 31 na kufungwa mabao manne tu.
Katika kipindi hicho ambacho kocha huyo amesimamia benchi la ufundi baada ya kujiunga nao akitokea Al Merreikh ya Sudan, Yanga imefunga jumla ya mabao 44 na imeruhusu nyavu zake kufungwa mara tisa tu.
Kutengeneza safu ngumu ya ulinzi ni jambo ambalo Nabi ameonekana amelimudu vyema ambapo chini yake wapinzani wameonekana kupata wakati mgumu kufania nyavu za kikosi chake na kudhihirisha hilo, kati ya mechi 26 ambazo Nabi ameiongoza Yanga katika Ligi Kuu tangu alipojiunga nayo, ana jumla ya mechi 19 bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa (clean sheets).
Lakini Nabi ili aweke rekodi hiyo ya ubabe kwenye Ligi Kuu hatokuwa na kibarua chepesi na badala yake atapaswa kutafuna mfupa mgumu ya mechi moja ya ligi ambayo timu hiyo itacheza katika siku zilizobakia kabla ya kocha huyo kutimiza muda wa mwaka mmoja.
Mechi hiyo ni dhidi ya Azam FC ugenini ambayo itachezwa mapema mwezi ujao baada ya kupisha mechi za timu za taifa zinazoendelea hivi sasa.
Aprili 6, Yanga itakuwa na kibarua dhidi ya Azam FC kwenye Uwanja wa Azam Complex kuanzia saa 1:00 usiku ambapo mbali na ushindi, Nabi bila shaka atataka kulipa kisasi kwa timu hiyo ambayo ndio pekee imemfunga kwenye Ligi Kuu tangu alipowasili nchini.
Baada ya hapo itakuwa na mechi za mashindano ya Kombe la Shirikisho la Azam na itarudi tena kwenye kibarua cha Ligi Kuu kwa kuvaana na watani wao Simba kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Aprili 30 ingawa muda huo tayari Nabi atakuwa ameshatimiza muda wa mwaka mmoja tangu atue.