Timu ya Young Africans itacheza mchezo wa Kimataifa wa Kirafiki dhidi ya Timu ya taifa ya Somalia iliyoweka kambi nchini Tanzania kujiandaa na mchezo wa hatua ya awali ya kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika 2023 dhidi ya Eswatini (Swaziland).
Young Africans watautumia mchezo huo Utakaopigwa Uwanja wa Azam Complex Chamazi Jijini Dar es salaam Jumamosi (Machi 12), kama sehemu ya kujiandaa na Mpambano wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya KMC FC.
Young Africans watakipiga na KMC FC Uwanja wa Benjamin Mkapa Machi 19, huku wakiongoza Msimamo wa Ligi Kuu kwa tofauti ya alama 08 dhidi ya Mabingwa Watetezi Simba SC.
Msemaji wa Young Africans, Haji Sunday Ramadhan Manara amesema maandalizi ya mchezo huo yanaendelea vizuri na wana imani kubwa kikosi chao kitapata wakati mzuri wa kujiandaa na mbio za kusaka alama tatu dhidi ya KMC FC.
“Tuko kwenye kiwango cha juu sana hivi sasa, kwa hiyo hatuwezi kukaa wiki nzima ikapita hivi hivi bila wachezaji wetu kucheza, na hata wale ambao hawajacheza mchezo wowote nao wapate angalau dakika fulani za kucheza. Mara nyingi wachezaji wakikaa muda mrefu bila kucheza wakirudi ni kama wanaanza upya,” amesema Manara.
Ameongeza Young Africans itaingia kambini leo Alhamis (Machi 10) kujiandaa na mchezo huo wa kirafiki pamoja na mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya KMC utakaochezwa Machi 19, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini.
Hata hivyo nyota wa Young Africans jana Jumatano (Macho 09) asubuhi walifanya mazoezi ya gym chini ya Kocha Msaidizi, Cedrick Kaze.
“Tumeanza kufanya mazoezi ya gym, wachezaji wote wanaendelea vizuri na tumeanza na mazoezi haya ili kuwaweka sawa,” amesema Kaze.