Klabu ya Young Africans imetoa tahadhari kwa klabu nyingine za Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kuzitaka zijitayarishe kwa vipigo kama ilivyokua katika Duru la Kwanza la Ligi hiyo.
Young Africans ndio klabu pekee ambayo haijapoteza mchezo katika Ligi Kuu msimu huu, huku ikiongoza msimamo kwa kufikisha alama 45, ikifuatiwa na Mabingwa Watetezi Simba SC wenye alama 37.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya hiyo Kongwe katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati Hassan Bumbuli amesema: “Tulipokua tunaanza msimu huu sisi Young Africans tulisema kwamba kila mchezo ni Fainali, lakini tunapoendelea na Duru hili la pili tunasema kila mchezo ni Fainali na Nusu, kwa maana hiyo tunaongeza uzito katika kila mchezo tunaokwenda kuucheza.”
“Dhamira hii ni sehemu ya kutaka kutimiza malengo yetu ya kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara msimu huu 2021/22 kwa kushinda kila mchezo ulio mbele yetu kwa sasa, tunaamini hili litawezekana kutoka na ushirikiano mkubwa tunaoupata kutoka kwa Mashabiki na Wanachama wetu.”
“Tumejizatiti kuongeza nguvu mara mbili zaidi ya ilivyokua kwenye Duru la kwanza, hivyo kwa yoyote ambaye hajacheza na Young Africans anapaswa kujiandaa na hiki ninachokisema hapa.”
Kauli hiyo ya Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Young Afrcans Hassan Bumbuli imekuja, huku kikosi chao kikijiandaa na mchezo wa Mzunguuko wa 18 wa Ligi Kuu dhidi ya KMC FC utakaochezwa kesho Jumamosi (Machi 19), katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, saa moja Usiku.
Mchezo wa Duru la kwanza uliozikutanisha timu hizo mjini Songea Mkoani Ruvuma katika Uwanja wa Majimaji, Young Africans ilifanikiwa kuchomoza na ushindi wa 2-0, mabao yakifungwa na Kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Mshambuliaji Fiston Kalala Mayele.
Young Africans inaongoza msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na alama 45 iliyozivuna katika michezo 17 waliyocheza hadi sasa, huku KMC FC ikishika nafasi ya 07 ikiwa na alama 22