MKAZI wa jijini Dar es Salaam, Borgias Kwitega, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa tuhuma za kumwekea dawa za kupumbaza mwanamke, kumbaka na kuiba simu.
Kwitega na mshtakiwa Abdallah Mmanyi ambaye anakabiliwa na shtaka la kupokea mali ya wizi, wamefikishwa jana mahakamani mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ramadhani Rugemarila na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Lucy Uisso.
Mshtakiwa wa pili Ally Kibuga, hakufikishwa mahakamani hapo, kwa kile kilichoelezwa kuwa bado yupo mikononi mwa polisi.
Wakili Uisso alidai washtakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 64/2022 na katika shtaka la kwanza, Kwitega anadaiwa kumwekea vidonge vya kupumbaza mwanamke.
Inadaiwa tukio hilo alitenda Januari 24, 2022 eneo la Rumix Hotel iliyopo Kinondoni, alimpa vidonge vya kupumbaza, mwanamke mwenye umri wa miaka 30.
Shtaka la pili, siku na eneo hilo, Kwitega alimbaka mwanamke huyo, bila ridhaa yake.
Shtaka la tatu, Kwitega anadaiwa kuiba simu aina ya iPhone yenye thamani ya Shilingi milioni tatu pamoja na nguo zenye thamani ya Sh. 300,000, vyote vikiwa na thamani ya Sh milioni 3.3.
Shtaka la nne ni kupokea mali ya wizi tukio, linalowakabili mshtakiwa Kibuga na Mmanyi.
Wakili Uisso, alidai washtakiwa hao wanadaiwa katika tarehe tofauti mwaka 2022, walipokea simu aina ya iPhone huku wakijua kuwa mali hiyo ni ya wizi.
Upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika na wanaomba tarehe nyingine.
Hakimu Rugemarila alitaja masharti ya dhamana kuwa kila mshtakiwa anatakiwa kusaini hati ya dhamana ya Shilingi milioni mbili.
Pia, washtakiwa hao wanatakiwa kuwa na wadhamini wawili wenye barua za utambulisho kutoka Serikali ya Mitaa.
Hata hivyo, washtakiwa hao wameshindwa kutimiza masharti ya dhamana na kurudishwa rumande.