Ajitosa Baharini na Kufa Akiwakimbia Polisi Kwa Tuhuma za Kutishia Kumuua Mpenzi Wake



MKAZI wa mtaa wa Sabasaba, Kata ya Jamhuri, Manispaa ya Lindi, Hassani Mussa M’buyu (27), amekufa maji, baada ya kujitosa baharini kwa madai ya kukimbia kukamatwa kwa tuhuma za kutishia kumuua mpenzi wake.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, ACP Mtatiro Kitinkwi, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Alisema M’buyu ambaye ni mwendesha bodaboda, alichukua uamuzi huo, Aprili 4, mwaka huu, saa 12:30 jioni.

Kamanda Kitinkwi alisema, M’buyu alifikishwa Kituo cha Polisi Lindi mjini kwa tuhuma za kumpiga na kumtishia kumuua mpenzi wake Sharifa Zakaria Mussa (23).

Alisema baada ya mlalamikaji kuwasilisha madai hayo, askari kupitia dawati la jinsia lilichukua jukumu la kumuandikia M’buyu barua kumtaka kufika kituoni kwa mahojiano kuhusu madai yaliyowasilishwa na mpenzi wake.


“Huyu M’buyu baada ya kufika kituoni pale, alielekezwa aende chumba cha dawati la jinsia,” alisema Kamanda.

Kamanda alisema baada ya mlalamikiwa kufika mlango wa chumba cha dawati, alimkuta mpenzi wake akiwa ndani ameshawasili na kuamua kuchukua hatua ya kukimbia, askari walivyomuona walimkimbiza, lakini alikataa kusimama na kujitosa baharini na kufariki.

“Kituo chetu cha polisi hapa Lindi mjini kipo kama umbali wa mita 100 kufika baharini,” alisema Kitinkwi.

Sharifa akizungumza na mwandishi wa habari hizi, alisema yeye na M’buyu walikuwa wapenzi na kubahatika kubeba ujauzito, lakini hakuwa anampatia huduma yoyote.

Alisema hata alipolazwa hospitalini akisumbuliwa na maumivu ya tumbo hakuwahi kwenda kumuona kumjulia hali, huku gharama zote za matibabu zikitekelezwa na mama yake mzazi, hatua iliyomlazimu kukatisha mahusiano yao.

Sharifa alisema uamuzi huo ulimjengea uhasama na mpenzi wake kwa kumpa kichapo na kumtishia kumuua iwapo ataendelea na uamuzi wake wa kumkataa kwa kumkata mapanga, hali iliyomlazimu kwenda kituo cha polisi kutoa taarifa ya usalama wa maisha yake.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad