Mwanza. Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza amesema kuna umuhimu wa Watanzania kuwa tayari kufikia muafaka katika mambo ya msingi yanayoibua misigano kwa nia ya kuendelea kuwa Taifa lenye watu wamoja licha ya tofauti zao kisiasa, kijamii na kiuchumi.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu leo Ijumaa Aprili 8, amesema ili kufikia lengo hilo, ni lazima kila upande unaohusika uweke mbele maslahi ya jamii na Taifa kwa ujumla kwa kukubali kupata na kupoteza kwa faida ya wote.
“Taifa limegawanyika. Karibia kila eneo kunasikika kauli za wao na sisi. Siyo kwenye siasa pekee, bali pia hata kwetu viongozi wa dini tumeparaganyika, na kwa msingi huo, ni dhahiri tunahitaji miafaka na siyo muafaka,” amesema Askofu Bagonza
Akithibitisha na kufafanua ujumbe wake unaozunguka kupitia mitandao ya kijamii yenye kichwa cha habari “Inahitajika miafaka, siyo muafaka’, Askofu Bagonza amesema ni ukweli usiopingika kwamba mparaganyiko unaoshuhudiwa nchini hivi sasa hauko kwenye uwanja wa siasa pekee kati ya walioko madarakani na walioko nje ya madaraka, bali uko katika kila kundi la jamii, hali inayolazimisha uwepo wa miafaka mingi kutibu Taifa.
"Katika kufikia miafaka hiyo, siyo lazima kukubaliana kila kitu kwa sababu muafaka siyo kukubaliana kila kitu, bali ni kukubaliana kutokukubaliana bila kuparaganyika," amesisitiza kiongozi huyo wa dini.
Soma ujumbe mzima wa andiko la Askofu Bagonza
INAHITAJIKA MIAFAKA siyo MUAFAKA
Kuna harufu ya mparaganyiko kila mahali. Ni kama tuna nchi moja yenye mataifa mengi ndani yake. Badala ya muafaka wa kitaifa, inahitajika miafaka kadhaa ili kuunda muafaka mmoja.
1. CCM si moja. Kuna CCM-Mpina na CCM-January. Kuna CCM-Mwendazake na CCM-Samia. Kuna CCM-Asili na CCM-Yatima. Hizi CCM zote zinahitaji muafaka ili tupate CCM moja.
2. Wapinzani si wamoja. Kuna wapinzani-Katiba Mpya na Wapinzani-Nusu Katiba Mpya. Kuna wapinzani-Mtungi na Wapinzani-Mahela. Kuna Wapinzani-Zanzibar huru na Wapinzani-Zanzibar Mkoa. Unahitajika muafaka kati ya wapinzani kabla ya muafaka wa kitaifa.
3. Serikali si moja. Kuna serikali awamu ya 5 rais wa sita na Serikali awamu ya sita rais wa sita. Kuna serikali-2025 na Serikali-2030. Hizi serikali zinahitaji muafaka.
4. Kuna bunge-live na bunge-giza. Kuna bunge-haramu ndani jengo halali na bunge-halali nje ya jengo halali. Kuna sheria halali zilizotungwa na bunge haramu.
5. Kuna Polisi-Tii sheria bila shuruti na Polisi-Tii shuruti bila sheria. Kuna IGP bila Polisi na Polisi bila IGP.
Unashangaa? Tanzania ni eneo la utalii. Kila kitu ni kiburudisho. Hatuambukizani Corona, tunaambukizana tabia. Mwenyekiti wa msiba anamuiga Spika namna ya kuongoza kikao cha mazishi. Askofu anamuiga OCD ili kuongoza kanisa. Kocha wa Simba anamuiga kocha wa Yanga lakini anafungwa mengi kuliko Yanga.
Bei ya mafuta imepandisha hata rushwa ya barabarani.
Mwananchi