Bandarini Kwapanguliwa, Vigogo Wahamishiwa Wizarani



Bandari Dar es Salaam Tanzania
MAGEUZI makubwa ya kimfumo na kiutawala yameanza kufanyika ndani ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa vigogo kadhaa kuondolewa kwenye nyadhifa zao. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Wanaotajwa kung’olewa ni Naibu Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi Karim Mataka, Freddy Liundi, aliyekuwa Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano na msaidizi wake, Lidya Mallya.

Mwingine ni Mkurugenzi wa Ununuzi na Usimamizi wa Mikataba, Charles Mnyeti na aliyekuwa Meneja wa Ununuzi aliyefahamika kwa jina moja la Macha.

Wakurugenzi hao wawili; Mhandisi Mataka na Liundi wanatajwa kuhamishiwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi siku chache baada ya Waziri Profesa Makame Mbarawa, kuonesha kutoridhishwa na watendaji hao.


Profesa Mbarawa alionesha shaka hiyo tarehe 18 Machi 2022, akizindua Bodi ya Wakurugenzi wa TPA, inayoongozwa Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) mstaafu Balozi Ernest Mangu akiitaka kwenda kusimamia taasisi hiyo kwa jicho la kipekee.

Aidha, alivitaja vitengo vya idara ya ununuzi na masoko, akisema bado havijatekeleza majukumu yao kwa ufanisi, huku akiitaka Bodi hiyo mpya kuangalia sekta hizo kwa ‘jicho la tatu’.
MwanaHALISI Online limedokezwa, kwamba Mhandisi Mataka ameshariwa kustaafu kwa hiyari, badala ya kuhamia wizarani ambako atasubiri kupangiwa kazi nyingine, kwani umri wa kustaafu kwa hiyari umefika.

“Baada ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Eric Hamisi kutembelea karakana kuu na kukuta vipuli vimefichwa na vingine kutoroshwa, ilibidi kumsimamisha mtendaji huyo wa ununuzi kupisha uchunguzi,” alieleza kiongozi wa chama cha wafanyakazi bandarini akiomba hifadhi ya jina lake.


Mtandao huu umedokezwa baada ya vigogo hao kuwekwa kando, kumekuwa na vikao vikiwamo vya Menejimenti na cha Bodi kujadili maagizo ya Waziri Mbarawa na ya Rais Samia Suluhu Hassan, kupata watu wa kuchukua nafasi zao.

“Tutaendelea kusikia mabadiliko ya kimfumo na kiutendaji, Mkurugenzi wetu anataka kuiweka sawa ofisi yake, kama alivyoagizwa kipindi anateuliwa na Rais.

“Sasa usishangae ukiwa unasikia fulani kahamishwa, fulani kapelekwa wizarani au kwingineko,” alidokeza mmoja wa viongozi wa juu aliyepo kwenye Menejimenti.

Jitihada za kumpata Mkurugenzi Mkuu wa TPA, kuzungumzia mageuzi hayo na kinachoendelea, bila mafanikio kwani kila alipopigiwa simu iliita na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi hakujibu.


MwanaHALISI Online lilidokezwa, kuwa baada ya vikao kufanyika, Placidius Mbosa atakaimu nafasi ya Mhandisi Mataka ya unaibu mkurugenzi mkuu.

Taarifa zaidi zilisema kutoka ndani ya TPA kuwa mageuzi hayo yanafanyika hivi sasa na yataendelea, ili kutekeleza maelekezo ya Rais Samia ya Desemba mwaka jana alipotembelea bandari hiyo na kubaini hali si shwari.

Hivi karibuni katika mahojiano na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Rais Samia aligusia mageuzi ya kimfumo na kiutawala ndani ya TPA, kwa lengo la kuboresha ufanisi zaidi ya sasa, ili kuchangia uchumi wa Taifa.

Mmoja wa viongozi wa wafanyakazi wa bandarini alisema, “Mkurugenzi Mkuu (Eric Hamisi) aliwapa nafasi watendaji wote aliowakuta na hakutaka kubadilisha mtu atakayeendana na kasi na maelekezo ya Serikali ya Rais Samia. Aliwaambia wazi kwamba wanaotaka kufanya kazi wabadilike.


“Mkurugenzi Mkuu aliwapa mamlaka kila mmoja katika nafasi yake na kuwapa ushirikiano mkubwa. Sasa wengine wakamwona ni dhaifu na wao wanastahili kukaa nafasi yake,” aliongeza.

Hamissi aliteuliwa na Rais Samia Aprili 5 mwaka huu, kuchukua nafasi ya Mhandisi Deusdedit Kakoko aliyewekwa kando kupisha uchunguzi wa tuhuma zinamkabili. Mpaka sasa, haifahamiki uchunguzi umefikia wapi.

Rais Samia alipomteua Hamissi akitokea Mwanza alikokuwa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), alimtaka kuunganisha wafanyakazi waliogawanyika pande mbili.

“Unajuana na watu wa Dar es Salaam, nenda pale usiangalie mtu usoni, najua ndani ya Bandari kuna makundi mawili, kuna makundi hili na lile, unakwenda pale huna kundi,” Rais Samia alimweleza Hamissi, Aprili 6 siku moja baada ya kumteua.

Miongoni mwa mabadiliko ambayo tayari Hamissi alifanya ni pamoja na kupangua baadhi ya watumishi, hali iliyosababisha kuanza kuleta ufanisi.


Mabadiliko hayo yanaelezwa kuchangia kupandisha mapato kati ya Julai mwaka jana na Februari mwaka huu, yaliyofikia Sh bilioni 704 ikilinganishwa na Sh bilioni 570 kipindi kama hicho mwaka jana.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, lengo la TPA la muda mrefu la kufikia Sh trilioni moja kwa mwaka, litafikiwa mara ya kwanza mwaka huu kutokana na maboresho na mabadiliko yanayoendelea.

“Walipoondolewa washika fedha na wahasibu wengi kwa mkupuo, watu walidai mapato yatashuka, lakini kumbe yamepanda maradufu. Inaonekana kulikuwa na mchezo mchafu,” alisema mmoja wa vigogo waandamizi wa TPA.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad