Benard Morrison Aitia Simba Hasira kwa Orlando



KITENDO cha winga Mghana Bernard Morrison, kutoruhusiwa kuingia nchini Afrika Kusini, hivyo kutarajiwa kuikosa mechi ya marudiano ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Orlando Pirates, kimeongeza hasira na ari kwa Klabu ya Simba kupania kumalizia mechi nyumbani.

Morrison yuko kwenye hatihati ya kutosafiri na timu hiyo kwenye mechi ya marudiano dhidi ya Orlando Pirates Aprili 24, mwaka huu kutokana na kuwa na matatizo kwenye Idara ya Uhamiaji ya Afrika Kusini.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez, akizungumza na mwandishi wetu jana alisema ni kweli Morrison ana matatizo na idara hiyo, hivyo ni ngumu kuingia nchini Afrika Kusini, lakini kwa sasa wanalishughulikia suala hilo ili wasafiri naye.

"Kuna ukweli, na hili ni bora tuliweke wazi, ni kweli alipata changamoto huko nyuma, unajua ana familia kule, alipata changamoto kwenye idara ya uhamiaji, na hili bado tunaendelea kulitatua, kikubwa ni lazima tufuate sheria za nchi na kusikiliza nini uhamiaji watasema, tukifanikiwa atakwenda na sisi.

"Ndiyo maana shughuli yote tunataka tuimalize tarehe 17 nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa, ya marudiano iwe ya kumalizia tu," alisema Barbara.


Alisema malengo yao ni kuhakikisha wanapata mabao ya kutosha katika mechi hiyo ya awali nyumbani, katika mchezo wa marudiano kazi iwe kulinda ushindi wao tu.

Barbara aliamua kuweka wazi hilo kutokana na minong'ono ya muda mrefu kuhusu mchezaji huyo kutoruhusiwa kuingia Afrika Kusini, sababu mbalimbali zikitajwa, na hii ni baada ya kutosafiri kwake na timu hiyo ilipokwenda kucheza mechi ya kwanza ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita nchini humo iliyochezea Mei 15 mwaka jana dhidi Kaizer Chiefs.

Morrison aliwahi kuishi Sauzi, akiichezea Orlando Pirates msimu wa 2016 hadi 2018, alipotimkia DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, kabla ya kutua Yanga mwaka 2000, akicheza nusu msimu na kujiunga na Simba.


Wakati huo huo, Kocha wa Makipa wa Simba, Tyron Damons, amesema atakabidhi faili la Orlando Pirates baada mechi zao za Ligi Kuu, kwa kuwa anajua vema timu hiyo ya nchini kwao Afrika Kusini.

Damons ambaye ni raia wa Afrika Kusini amewahi kuziongoza timu kadhaa kucheza dhidi ya Orlando Pirates kwenye Ligi Kuu ya nchini humo, ikiwamo TS Galaxy na Bidvest Wits.

Akizungumzana gazeti hili jana, kocha huyo wa makipa Simba, alisema Orlando Pirates ni timu nzuri lakini ana imani wachezaji wao wakifuata yale wanayopewa mazoezini ana imani kubwa watasonga mbele na kucheza nusu fainali.

“Naifahamu Orlando Pirates, lakini pia tunaweza kupata taarifa zao kutoka Afrika Kusini na baada ya mechi dhidi ya Coastal Union, tutakaa na Kocha Pablo (Franco) kuangalia ubora na udhaifu wa wapinzani wetu,” alisema.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad