KWENYE mechi mbili za hivi karibuni ambazo Simba imecheza dhidi ya US Gendarmerie ambayo ilikuwa ni ya Kombe la Shirikisho, pamoja na ile ya Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union imeonyesha kuwa timu hiyo inatengeneza nafasi nyingi za kufunga, lakini kwa bahati mbaya hazitumiwi vizuri.
Licha ya kushinda mabao 4-0 kwenye mechi hiyo ya mwisho wa makundi, wachezaji wa Simba walitengeneza nafasi nyingi hasa kipindi cha kwanza, lakini walishindwa kuuweka mpira wavuni.
Hiyo iliwaweka juu wanachama na mashabiki wa timu hiyo, mpaka pale walipojirekebisha kipindi cha pili na kufanikiwa kupata mabao na kwenda kwenye hatua ya robo fainali.
Kwenye mechi dhidi ya Coastal Union hali iliendelea kuwa vile vile. Ilitengeneza nafasi nyingi za kufunga, hasa kipindi cha pili wapinzani waliposawazisha, lakini wachezaji wa timu hiyo walionekana kuwa na matatizo wanapofika karibu na lango, mpaka pale Meddie Kagere alipoweka bao la pili dakika za majeruhi.
Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola akakiri kuwa wamekuwa na udhaifu huo wa kukosa mabao mengi ya wazi.
"Suala hili tumekuwa tukilifanyia kazi sana kwenye uwanja wa mazoezi. Lakini tutaendelea kurekebisha ili kupata mabao mengi kwenye mechi, kwa sababu tunatengeneza nafasi nyingi, ila kuzitumia tu ndiyo tatizo," alisema Matola.
Ukiingalia Simba ni moja kati ya timu inayotengemeza nafasi nyingi si kwenye mechi hizi mbili tu, bali tangu msimu huu umeanza.
Ila kwa bahati mbaya mastraika wake wameshuka viwango vya kutumbukiza mpira ndani ya wavu.
Kinachotakiwa kwa sasa ni kusaidiwa tu kuweza kupata nafasi rahisi za kufungwa na si vinginevyo.
Simba ambao ndiyo wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa, inakwenda kucheza dhidi ya Orlando Pirates kwenye mechi ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF), Aprili 17, Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Marudio ya mechi hiyo watachezwa Aprili 24, nchini Afrika Kusini. Ni mechi ya mtoano ambayo Simba inaanzia nyumbani, hivyo inatakiwa imelize mechi hiyo mapema.
Nina maana inatakiwa ifunge mabao mengi iwezekanavyo. Lakini hayafungwi kwa domo, bali ni lazima vitu vifanyike.
Pamoja na yote, kufunga ni sanaa. Si kila mtu anajua kufunga. Kwa maana hiyo benchi la ufundi la Simba lingetafuta namna ya kufanya ili wapate mabao mengi.
Niliona kwenye mechi didi ya US Gendarmarie, kulikuwa na namna fulani ya uchoyo kwa baadhi ya wachezaji wa Simba, ambao kila mmoja akifika golini anataka kupiga tu ili afunge. Hakuna bao linalofungwa namna hiyo.
Mpira ni mchezo wa ushirikiano, haiwezekani mchezaji yupo pembeni kidogo mwa lango anataka kulazimisha kufunga badala ya kumpa mchezaji mwenzake.
Bernard Morrison, ndiye aliyeongoza kwa kuingia ndani ya boksi na kukosa mabao. Hata kwenye mechi dhidi ya Coastal ni hivyo hivyo. Matola anasema analifanyia kazi suala hilo yeye na kocha wake mkuu, Pablo Franco.
Mimi nitoe ushauri tu kuwa kama watamtumia Morrison vizuri, Simba inaweza kupata mabao kuanzia matatu hadi matano kwenye mechi ya kwanza.
Kwanza kabisa ni lazima aanze, kwa sababu ni mchezaji mwenye uthubutu, ambaye akipata mpira anachojua ni kulitafuta eneo la wapinzani na si kuangalia, au kurudisha mpira nyuma.
Atengenezwe kuwa mpishi wa mabao kwa wenzake, ambao naona wanaweza kufunga mabao rahisi sana na mengi.
Akipata mpira huwa mtata, kwa kupiga chenga za maudhi na kuingia ndani ya hatari, lakini tatizo hutaka kufunga mwenyewe, huku wenzake wakiwa wanamtazama tu.
Pamoja na uwezo wake huo mkubwa, Morrison hata sanaa na kufunga mabao. Angekuwa anatengenezwa kupiga krosi na kutoa pasi za mwisho kila anapopata mpira, basi Simba ingevuna mabao mengi sana.
Kwenye mechi dhidi ya Orlando Pirates, benchi la ufundi la Simba linatakiwa kumuambia kuwa yeye asiwe mfungaji kwenye mechi hiyo, bali ni mtoa pasi za mwisho tu na si vinginevyo.
Akipewa kazi hiyo, kwa sababu anafuatwa na mabeki wengi, inaweza kuwa nafuu na mastraika wa Simba na wengine wakijazana golini kuweka mipira ndani ya wavu.
Morrison si muoga wa kulitafuta boksi, hivyo anatakiwa awe anawavuta, na yeye akatoa pasi ambazo zitawakuta wenzake wako kwenye eneo sahihi kwenye mapana ya goli na kufunga mabao rahisi.
Hii itawafanya kupata mabao mengi, ambayo yatawaweka salama kuelekea kwenye mechi ya marudiano Sauzi.