KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdallah Bulembo, amemuomba Makamu Mwenyekiti wa chama hicho bara, Abdulrahman Kinana, kumhoji na kumchukulia hatua za kinidhamu Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina kwa madai ya kwenda kinyume na maadili ya chama.
KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdallah Bulembo.
Bulembo amesema hatua ya Mpina kuongea hadharani akimshutumu Waziri wa Nishati, January Makamba, kwamba uamuzi alioufanya wa kuondoa tozo ya Sh. 100 kwenye lita ya mafuta ulikuwa ni wa uhujumu uchumi, vyombo vya uchunguzi vifanye kazi yake haikuwa kauli nzuri.
Juzi, Mpina akizungumza na waandishi wa habari alisema Waziri wa Nishati, Makamba hakufuata utaratibu wa kisheria wa kuondoa tozo ya Sh. 100 kwa lita ya mafuta, hakupata baraka kutoka bungeni na mchakato wake ulikuwa batili.
Mpina alisema tozo hiyo ya mafuta ipo kisheria katika bajeti ya serikali ya mwaka 2021/22, Waziri Makamba alivunja Katiba ya nchi na hakuwa na mamlaka ya kuondoa tozo hiyo iliyopitishwa na Bunge.
Pia, Mpina alitaka Waziri Makamba kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwamo kushtakiwa kwa uhujumu uchumi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kuanza kumhoji waziri huyo kwa kosa la kuingizia hasara Taifa Sh. bilioni 30 kwa mwezi Machi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Bulembo alisema: “Mpina ni mbunge wa CCM, CCM ina vikao vya ndani vya chama ambavyo vinatumika kuwekana sawa pindi mmoja anapokwenda ndivyo sivyo, sasa yeye (Mpina) kwa nini hakutumia vikao vya chama hadi anazungumza hadharani.”
“Yeye ni mbunge, angezungumzia suala hilo ndani ya Bunge na siyo nje. Namuomba Kinana aanze na Mpina kwa kitendo alichokifanya cha kumshambulia Waziri Makamba hadharani, huko ni kukosa maadili.”
Bulembo ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM, alisema suala la kuondolewa tozo ya Sh. 100 kwa lita ya mafuta lilishatolewa ufafanuzi na Rais Samia Suluhu Hassan ambaye alitangaza kuirejesha, Mpina hakupaswa kulizungumzia tena suala hilo.
Aliongeza kuwa hata suala la kuchelewa kukamilika kwa mradi wa bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere, Mpina hakupaswa kulizungumzia kwa sababu Rais Samia alishalizungumzia kuwa limechelewa na litakamilika mwaka 2024.
“Kinana hili suala lazima alichukulie hatua. Mpina hawezi kuivua nguo CCM hadharani angetumia vikao vya chama kuzungumza hayo aliyoyasema. Ninaamini kile alichokisema Mpina, Kinana amekisikia na amekiona na atachukua hatua za kinidhamu kwa mujibu wa Katiba ya CCM,” alisema Bulembo.
Alisema Mpina ni mbunge wa muda mrefu, ni mwanachama wa CCM mzoefu ambaye anafahamu miiko na taratibu za chama na sehemu sahihi ya kuzungumzia na kuwa kitendo alichokifanya kitawafundisha wanachama wadogo wa CCM kuzungumza kiholela pasipo kufuata utaratibu uliowekwa kichama.