CAF, TFF zabariki Mashindano ya Quraan kuunguruma Uwanja wa Mkapa



Shirikisho la soka Barani Afrika ‘CAF’ limeafiki mashindano makubwa ya Quraan kufanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa siku ya Jumapili (April 17), licha ya uwepo wa mchezo wa Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Simba SC itakua mwenyeji wa mchezo wa Robo Fainali Kombe la Shirikisho siku hiyo dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini kuanzia saa moja jioni.


‘CAF’ wameafiki shughuli za mashindano hayo kuendelea Uwanjani hapo, baada ya kufanya kikao na Shirikisho la soka nchini Tanzania ‘TFF’ pamoja na waratibu wa mashindano hayo na kufikia muafaka.


Meneja wa Habari na Mawasilino ya Simba SC Ahmed Ally amesema: “Maswali yamekuwa mengi kuhusu Uwanja wa Mkapa sababu siku ya mchezo dhidi ya Orlando Pirates kutakuwa na mashindano makubwa ya Quraan, na inafahamika kwamba uwanja unatakiwa kuwa wazi kwa masaa 72 kabla ya mchezo. Baada ya mazungumzo baina ya Simba, CAF, TFF na waandaaji wa mashindano ya Quran tumekubaliana matukio yote yatafanyika ndani ya siku hiyo moja na CAF wamebariki hilo.”


Simba SC ilitinga Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika ‘CAF’ kwa kishindo, kufuatia kisago kilichoishukia USGN ya Niger cha 4-0 Jumapili (April 03), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.


Simba SC ilimaliza nafasi ya pili kwenye Kundi D ikiwa na alama 10 sawa na RS Berkane ya Morocco, huku ASEC Mimosas ya Ivory Coast na USGN ya Niger zikitupwa nje ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad