CCM inavyokirudisha chama kwa wenyewe



Dodoma. Chama kinarudi kwa wenyewe, ndicho kinachosemwa juu ya marekebisho ya katiba yanayotarajiwa kufanywa kesho katika Mkutano Mkuu Maalumu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) jijini Dodoma.

Miongoni mwa marekebisho yatakayofanyika kesho ni kuwarejesha kwenye Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) makatibu wa mikoa ambao waliondolewa kuingia kwenye vikao hivyo mwaka 2017 pamoja na kuwapa majukumu ya kufanya wajumbe wa Nec kuanzia ngazi za chini, mitaa na kata.

Dhana ya kukirejesha chama kwa wenyewe inatokana na ukweli kuwa makatibu wa mikoa ndio watendaji na watekelezaji wa maagizo kutoka Nec, hivyo kutohudhuria kwao kwenye vikao hivyo kunawanyima fursa ya kusikiliza na kujua moja kwa moja kilichojadiliwa na kukabalika kwenye vikao hivyo.

Pia sasa siasa za ushindani zitarejea kuanzia ngazi za chini kwa kuwa sasa CCM haizungumzii gharama kubwa za uendeshaji wa vikao kama ilivyokuwa mwaka 2017 wakati katiba iliporekebishwa na kupunguza idadi ya wajumbe wa kuhudhuria vikao.


 
Akizungumza na Mwananchi, Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Zanzibar), Dk Abdulla Mabodi alisema kuna mambo ambayo kikatiba yanatakiwa yakubaliwe na Mkutano Mkuu Maalumu ili itengenezwe katiba bora kwa ajili ya mipango ya chama.

“Naamini wajumbe watajadili yote kwa utulivu na umakini kwa ajili ya masilahi ya chama,” alisema.

Taarifa ambazo Mwananchi imezipata zinaeleza kuwa CCM wamebaini upunguzaji wa gharama walioulenga umewaathiri kwa kupunguza ufanisi na kusababisha mawasiliano kutoka ngazi moja kwenda nyingine kutofanyika kwa usahihi.


“Hivi kuna faida gani ya kupunguza gharama wakati wenzako wanazidi kuimarika kuanzia ngazi za chini? Sisi tumejifunza kutokana na makosa, tumebaini mambo mazuri yanahitaji gharama,” kilisema chanzo kimoja cha Mwananchi.

Wajumbe wa Nec wanapewa majukumu hayo ili kushirikiana kwa ukaribu na mabalozi wa nyumba 10 na wenyeviti wa mitaa kwa lengo la kukiimarisha chama na kukabiliana na upinzani ambao pia kadri siku vinavyokwenda ndivyo unavyozidi kuimarika kuanzia ngazi za chini.

Naye Katibu wa Itikadi na Uenezi Zanzibar, Catherine Nao alisema wanatarajia katiba nzuri itakayosheni vitu vizuri kwa chama na Jumuiya zake.

“Naamini Mkutano Mkuu Maalumu utafanya mabadiliko yatakayotuimarisha zaidi kulingana na wakati tulionao, CCM itaendelea kuimarika,” alisema.


 
Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM, Julius Kambarage alisema wajumbe wana furaha kuitwa kwa ajili ya kushiriki mkutano huo, utakifanya chama chao kiwe imara zaidi. Mbunge wa Mtera ambaye ni mjumbe wa NEC, Livingstone Lusinde (Kibajaji), alisema wanakwenda kupata CCM mpya itakayowavusha miaka mingi ijayo.

Dodoma ya kijani

Maeneo mbalimbali ya jiji la Dodoma yamepambwa kwa bendera zenye rangi ya kijani, huku baadhi ya nyumba za kulala wageni zikieleza kupokea idadi kubwa ya wageni.

Baadhi ya wafanyabiashara wameomba utaratibu katika ratiba ya mkutano huo isiwe kama baadhi ya mikutano ya hivi karibuni ambayo ilikuwa ikiendeshwa kwa nusu saa na kufungwa, kitendo wanachosema kiliwatia hasara.

Hadija Mungaa ambaye ni mama lishe alisema mikutano miwili mfululizo ilikuwa ni hasara kwake, kwani alikuwa akijiandaa kupika lakini kabla havijaiva akasikia ving’ora kwamba mkutano umekwisha.


Jebra Likomawage, anayeuza dawa za asili alisema anaamini watafanya biashara katika mkutano huo.

Taarifa ya nyongeza Habel Chidawali (Dodoma) na Jesse Mikofu (Zanzibar).

Mwananchi


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad