NIMEKUWA nikitazama majina ya mastaa wa Simba ambao wanamaliza mikataba yao mwishoni mwa msimu. Wengi ni mastaa hasa kikosini na nadhani Simba itawagharimu pesa nyingi kuwabakisha hasa wachezaji wa kigeni.
Simba wanaweza kutumia zaidi ya Sh200 milioni kuwabakisha mastaa waliopo achilia mbali kuleta mastaa wengine wapya kikosini. Nimeamua kutoa hukumu ya haraka kwa jinsi ninavyowaona mastaa wenyewe na mchango wao kikosini.
Aishi Manula? Lazima wapambane kuhakikisha anapata mkataba mpya. Ndiye kipa namba moja wa Simba na timu ya taifa. Niliandika wiki iliyopita kwamba Simba na Taifa Stars wamewekeza sana kwake kwa kumpatia mechi nyingi za kimataifa na sasa anaingia katika kundi la makipa wenye uzoefu mkubwa nchi hii.
Simba lazima wapambane kumbakisha Aishi kwa sababu kama wakimpoteza itachukua muda kwa lango lao kutulia kwa kipa mwingine. Afrika ina uhaba wa makipa wazoefu. Kama wanabisha waangalie jinsi ambavyo watani zao Yanga walivyopata shida kupata kipa wa kudumu. Kuna wakati walikuwa na makipa wanaopeana na zamu.
Joash Onyango. Kama ilivyo kwa Aishi. Utapata wapi mlinzi wa kati mwenye uzoefu katika njia rahisi kuziba nafasi ya Onyango? Lakini zaidi ni kwamba kombinesheni yake na Henock Inonga inakwenda vyema. Wakati mwingine walinzi ni suala la kombinesheni zaidi.
Joash alishatulia na Paschal Wawa, lakini alipoletewa Inonga ametulia naye pia. Haitakuwa jambo zuri kwa Simba kutafuta mlinzi mwingine wa kati wa kutengeneza kombinesheni na Inonga. Hauwezi kujua kama kombinesheni hiyo itakuwa imara kiasi gani. Joash lazima apewe mkataba mpya haraka iwezekanavyo. Ni miongoni mwa mabeki bora wa kati nchini.
Rally Bwalya? Huu ni mtihani. Kipaji kipo kwa Bwalya lakini hajawahi kuikamata Simba kama inavyotakiwa. Hata walipoondoka Luis Miquissone na Clatous Chotta Chama watu wengi walitazamia Bwalya avae viatu vyao lakini hakuvaa kama inavyotakiwa.
Bwalya anacheza soka laini, hana kasi, hana uamuzi wa haraka lakini pia ameshindwa kufunga mabao mengi au kutoa pasi nyingi za mwisho kama ilivyokuwa inadhaniwa. Simba inapotawala mechi basi na Bwalya anakuwa miongoni mwa mastaa. Inapokuwa na mechi ngumu basi na Bwalya anapotea.
Kwa mtazamo wangu Simba ikipata kiungo mwingine mzuri zaidi katika eneo la ushambuliaji basi wanaweza kuachana na Bwalya. Kama atahitaji pesa nyingi kwa ajili ya kusaini mkataba mwingine wa miaka miwili nadhani wanaweza kutulia kwanza na kutazama jicho lao kwingine. Hauwezi kulaumiwa na mashabiki kwa kuachana na Bwalya.
Meddie Kagere? Anamaliza mkataba wake, lakini kama unataka kutengeneza orodha ya washambuliaji watatu katika Simba basi Kagere lazima awepo. Mpaka sasa anaweza kuwa mshambuliaji namba moja klabuni baada ya John Bocco kuwa na msimu mbovu huku Chris Mugalu akiwa majeruhi kwa muda mrefu.
Unaweza kuachana na Mugalu lakini sio Kagere. Bocco ana faida ya kuwa mchezaji mzawa, lakini kama unataka kuongeza mshambuliaji wa kigeni halafu upunguze mmoja nadhani anayeweza kupisha nafasi ni Mugalu na sio Kagere.
Nafahamu kwamba Simba wana mpango wa kuongeza mshambuliaji mmoja wa kigeni na haitakuwa vyema kwao kuwa na washambuliaji wanne wa kariba ya juu. Kama mshambuliaji mmoja itabidi aondoke nadhani atakuwa Mugalu.
Hamis Dilunga? Aongezewe mkataba mpya. Ni miongoni mwa wachezaji wazawa ambao wamekuwa wakizipigania nafasi zao vyema kando ya Jonas Mkude, Shomari Kapombe, John Bocco, Mohamed Hussein na Aishi Manula.
Zaidi ya kila kitu ni kwamba Dilunga ni mzawa. Hana gharama kubwa kama wachezaji wa kigeni lakini hakuna nafasi anayoiziba kwa yeye kuendelea kuwepo kikosini, sanasana anaipa Simba machaguo mengi katika eneo la mbele.
Bernard Morrison? Nadhani ni jina ambalo litawasumbua watu wengi wa Simba wakati wakijadiliana wachezaji wa kigeni kuwaacha. Atawagawanya mashabiki na viongozi. Kipaji cha Morrison kipo wazi lakini na yeye kama alivyo kwa Bwalya kuna mahala bado hajafika.
Simba watahofia kwamba huenda wakimuacha Morrison basi atarudi katika klabu yake ya zamani na kuanza kuwasumbua. Hata hivyo namba zake tangu aingie Simba hazitasapoti mawazo yao. Kuna mechi kadhaa ambazo alionyesha kiwango kikubwa lakini kisha akazimika mechi zinazofuata.
Staa huyu ambaye analilia kuchezea timu yake ya taifa ya Ghana hana sababu za kuisumbua Simba hasa ukizingatia pia kwamba hapo katikati aliwahi kuwaletea Simba matatizo ya utovu wa nidhamu kama ambayo aliwahi kuyafanya na Yanga.
Simba wakipata mbadala mahiri wa Morrison nje ya nchi wanaweza kuachana naye. Suala ni kupata mbadala sahihi tu. Lakini pia Simba wakumbuke kwamba Peter Banda na Ousmane Sakho watakuwa wakiingia katika msimu wao wa pili Tanzania na huenda wakazoea zaidi. Sasa hivi tayari wameanza kuwa wa moto na msimu ujao tutegemee watakuwa wa moto zaidi.
Thadeo Lwanga. Injinia alikaa nje kwa muda mrefu na sasa amerudi uwanjani. Injinia ana staili yake ya kipekee katika timu na ni mchezaji ambaye Simba wanapaswa kumbakisha lakini huku wakitumia tahadhari fulani kuanzia sasa hadi mwishoni mwa msimu.
Simba inabidi wachunguze kama injinia ameendelea kuwa mchezaji yuleyule au vinginevyo. Wakati mwingine wachezaji wakikaa nje kwa muda mrefu kasi yao huwa inaathirika na hawarudi kuwa bora kama walivyo.
Kama injinia akirudi katika ubora wake basi wampe mkataba mpya. Anajua kunusa hatari na kukata umeme. Ni kitu muhimu ambacho pacha wake wa uwanjani Jonas Mkude hana. Lakini kama asiporudi katika ubora wake nafasi yake anaweza kutafutwa mtu mwingine.
Chris Shimba Mugalu? Kama Simba watapata mshambuliaji hatari mwenye namba nzuri za mabao nadhani wanaweza kuachana na Mugalu wakabakia na Bocco na Kagere. Hauwezi kuchukua mshambuliaji mwingine bila ya kumuacha mshambuliaji mmoja kati ya hawa.
Hauwezi kuwa na washambuliaji wanne wenye umri mkubwa na wenye majina makubwa klabuni. Kama ikitokea nani aondoke nadhani ataondoka mshambuliaji mmoja wa kigeni kwa ajili ya kupisha nafasi ya mshambuliaji mmoja wa kigeni klabuni. Ni hapo ambapo itabidi aondoke mmoja kati ya Kagere au Mugalu. Hapana shaka jibu la wengi ni Mugalu.
Makala haya yameandikwa na Edo Kumwembe na kuchapishwa kwanza kwenye wavuti la MwanaSpoti