FAMILIA ya aliyekuwa Mkuu wa Wamisionari Afrika nchini Tanzania, Padri Francis Kangwa, imesema imepokea kifo chake kwa kuwa ni baraka na kwamba wanasherehekea maisha yake ulimwenguni wakati alipokuwa hai. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Kauli hiyo imetolewa na familia hiyo katika mazishi ya Padri Kangwa, yaliyofanyika leo Alhamisi, tarehe 21 Aprili 2022, kwenye Kituo cha Hija cha Pugu.
“Hatutaki kubishana na Mungu, tumepokea kifo chake. Huu ni ujumbe kwa ulimwengu kwamba kifo cha Padri Kangwa ni baraka na tutasherehekea maisha yake,” amesema Kaka wa marehemu William Kangwa.
Familia hiyo imesema, haijali amefariki vipi, wapi na nani anayefahamu kuhusu kifo chake.
“Ujumbe wa Familia ya Kangwa ni kwamba tumepokea kifo cha Father Francis, hatujali vipi, wapi, nani anajua, hatuhitaji kujua,” imesema familia hiyo.
Awali Kaka huyo wa marehemu amesema wamepokea kifo cha ndugu yao akisema “ujumbe wetu kwenu, tumepokea taarifa za kuondoka kwa kaka yetu, hiyo ndiyo njia iliyohitimisha maisha yake. Tunamshukuru Mungu kwa muda aliompa wa kuwatumikia watu wake.”
William amelishukuru Kanisa kwa mapokezi mazuri waliyopewa walipotoka Zambia kuja Tanzania kushiriki mazishi ya ndugu yao.
Akielezea kwa ufupi maisha ya Hayati Padri Kangwa, kaka huyo amesema ndugu yao alikuwa msikilizaji, mkarimu na mwenye kutoa msaada kwa wahitaji hasa vijana.
Mwili wa Padri Kangwa, ulikutwa kwenye tanki la maji la nyumba ya mapadri iliyopo jengo la Ottoman jijini Dar es Salaam, tarehe 15 Aprili mwaka huu.